Maswali magumu Roma Mkatoliki

09Apr 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
Maswali magumu Roma Mkatoliki

WAKATI kukiwa na taarifa za madai ya kupatikana kwa nyota wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa (Roma Mkatoliki) pamoja na wenzake baada ya kutoweka kwa siku tatu, utata kuhusiana na tukio hilo umeibua maswali kadhaa magumu.

Awali, ilielezwa kuwa Roma na wenzake watatu, walitekwa kwa pamoja na watu wasiofahamika Aprili 5 mwaka huu.Watu watano wasiofahamika walidaiwa kufika kwenye studio ya Tongwe Records iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam mishale ya saa 5:40 usiku na kuondoka nao kuelekea kusikojulikana.

Wengine waliokumbwa na mkasa huo ni mtayarishaji wa kipindi aliyefahamika kwa jina la Moni, Bin Raida na Emmanuel.

Hata hivyo, Nipashe ilielezwa jana na mmoja wa watu wa karibu wa Roma kuwa msanii huyo na wenzake walipatikana mishale ya mchana walikuwa salama katika maeneo ya Oysterbay.

Pamoja na kuwapo kwa taarifa hiyo iliyosambaa pia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii jana, Nipashe haikuweza kupata tarifa rasmi za Polisi kuthibitisha taarifa hiyo.

Awali, mishale ya saa 5:00 asubuhi, Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa msanii huyo na wenzake walikuwa wakiendelea kutafutwa kupitia uchunguzi wanaoufanya na kuwataka wananchi watulie ili kuwapa nafasi ya kufanya uchunguzi wa suala hilo.

“Kimsingi kama ninavyosema siku zote, sipendagi kutoa majibu ya harakaharaka. Suala liko Polisi… tuache Polisi ishughulike.

Lakini sasa kuna watu wanakuwa zaidi ya Polisi. Wanataka kutuingilia sisi, na wanataka kuwa Kamishna Sirro anazungumzia habari ya upelelezi,” alisema Sirro.

MASWALI MAGUMU
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya mashabiki wa Roma na wafuatiliaji wa masuala ya usalama walisema sakata la msanii huyo limeacha maswali kadhaa magumu.

“Hili tukio la Roma Mkatoliki limeacha maswali mengi yanayohitaji majibu,” alisema mmoja wa mashabiki wa msanii huyo.

Kwanza, swali mojawapo muhimu lililotajwa ni kwamba je, msanii huyo alikuwa akirekodi wimbo wenye maudhui gani studio wakati akitekwea?

Swali la pili, ni kwamba je, wanaodaiwa kumteka Roma na wenzake ni watu gani? Maana inadaiwa walibeba pia kamera na vifaa vingine muhimu vya studio.

Swali tatu ni je, lengo la watekaji hao wa Roma na wenzake ni lipi? Nne ni je, waomteka Roma na wenzake walitumwa na nani? Na tano, kwa makusudi gani? Je, kulikoni wakamteka lakini simu yake ikadaiwa kuwa hewani huku ikipokea ujumbe mfupi na kuonyesha kuwa umesomwa kila ulipotumwa?

Maswali mengine ni pamoja na lile la kutaka kujua kuwa ni kwa nini wanaodaiwa kuwa watekaji walifanikisha tukio hilo studio na siyo sehemu nyingine?

Aidha, swali lingine ni kuhusiana na hofu juu ya uwezekano wa kutokea tena matukio mengine ya aina hiyo, hasa baada ya kutoweka pia kwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane ambaye hajulikani alipo tangu Novemba 8, mwaka jana.

ALICHOSEMA KAMANDA SIRRO
Awali, kabla ya kuwapo kwa taarifa za kupatikana kwa Roma na wenzake, Kamanda Sirro aliwaambia waandishi wa habari kuwa anashangaa kuona kuna baadhi ya watu wanaingilia shughuli za Jeshi la Polisi kuhusiana na suala hilo na kuwataka waache ili wao (polisi) wafanye kazi yao.

Alisema:”Nimeona kwenye mitandao mingi watu wanakutana na kuzungumza baada ya tukio hili kutokea.
Nikajiuliza kama kila tukio linapotokea watu wanakusanyana ingekuwaje? Hii kazi tunaifanya kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi, hivyo tunaomba tuifanye kazi hii,” alisisitiza Kamanda Sirro.

Pia alisema suala la utekeji wanalichukulia kama yanavyotokea matukio mengine ya ujambazi na uporaji, hivyo ni jambo ambalo linatafutiwa ufumbuzi.

“Nalichukulia kama tukio la kawaida la kutekwa na limeshawahi kutokea, na yanatokea kwa sababu majambazi yapo na ndiyo maana kuna Jeshi la Polisi… siwezi kusema kuwa hali ni mbaya kwa sababu ni jambo la kawaida sana,” alisema Kamanda Sirro.

Habari Kubwa