Marekebisho kodi kuvutia viwanda 

07Dec 2017
Augusta Njoji
Nipashe
Marekebisho kodi kuvutia viwanda 

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema serikali imeanza  kupokea mapendekezo ya kurekebisha ya mfumo wa kodi ili kuharakisha ujenzi wa viwanda.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango

Aidha, amesema katika maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha ya mwaka 2018/19, serikali imeona ni vyema kushirikisha sekta binafsi ili kupata mapendekezo ya kujenga uchumi imara kutokana na washirika wa maendeleo kupungua kila mwaka.

Dk. Mpango alisema hayo jana mjini hapa kwenye mkutano wa majadiliano wa masuala ya kodi kati ya serikali na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), kwa ajili ya maandalizi ya matayarisho ya bajeti ya mwaka 2018/19.Katika kikao hicho, serikali inatarajia kupata mapendekezo kutoka sekta binafsi ili kuwa na mfumo mzuri wa kupaisha uchumi wa nchi.

Waziri Mpango alisema serikali inatarajia kupata mapendekezo yanayotekelezeka katika mazingira ya sasa na ambayo yatafungulia nguvu za sekta binafsi.

“Lakini bila kuathiri uwezo wa serikali kutekeleza majukumu yake ya msingi, nitapenda nipate mapendekezo ya kurekebisha mfumo wa kodi ili kuharakisha ujenzi wa viwanda nchini,” alisema Dk. Mpango.

Aidha, alisema kwa madhumuni ya kuimarisha uhusiano kati ya serikali na sekta binafsi, pande zote zimekuwa zikifanya mikutano ya majadiliano, iliyo rasmi na isiyo rasmi kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini kwa kupunguza na baadaye kuondoa kabisa changamoto zinazoikabili sekta binafsi na kuifanya ichangie ipasavyo kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Itakumbukwa kuwa Aprili, 2017 tulifanya mkutano wa pamoja hapa Dodoma na Oktoba, 2017 pia tulifanya mkutano mwingine wa pamoja mjini Dar es Salaam. Mikutano yote miwili imekuwa na manufaa makubwa baina ya pande zote mbili kwa kuwa kupitia mikutano hiyo tumeona dhahiri ya kwamba tukikaa pamoja kwa umoja na kwa kusikilizana hakuna linaloshindikana,” alisema Mpango.

Alisema mkutano huo utajadili kwa kina masuala yanayohusu kodi peke yake kabla ya kufanya mkutano mwingine wa ujumla.

“Serikali iko tayari kupokea maoni na mapendekezo yanayohusu masuala ya utozaji kodi na usimamizi wa kodi kutoka kwenu ili kuweza kuboresha mfumo mzima wa kodi hapa nchini,eneo la maboresho ya sera na sheria za kodi nchini yanalenga kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mpango alisema kumekuwa na kushuka kwa mikopo ya masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo Sh. trilioni 1.3 mwaka 2013/2014 hadi Sh. bilioni 495 kwa mwaka 2015/16.

Aidha, alisema kwa upande wa misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo imeshuka kutoka Sh. Trilioni 1.5 kwa mwaka 2013/14 hadi Sh. Trilioni 1.23 kwa mwaka 2015/16.

Alisema kutokana na misaada hiyo na mikopo kupungua wananchi hawapati mahitaji ya msingi ikiwemo huduma za kijamii.

“Uzalishaji wa maji katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo ni lita milioni 99.5 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 273 kwa siku, (sawa na asilimia 36.4). Miradi ya maji ya Kitaifa uzalishaji ni lita milioni 59.5 ikilinganishwa na mahitaji ya lita 119 kwa siku. (sawa na asilimia 50 ya mahitaji),” alisema.

Kuhusu sekta ya Afya, Dk. Mpango alisema vifo vitokanavyo na uzazi ni 556 katika kila vizazi hai 100,000 wakati lengo ni kuvipunguza visizidi vifo 265 katika kila vizazi hai 100,000 itakapofika mwaka 2020.

“Nchi yetu bado inategemea wafadhili kwenye dawa kwa kiasi kikubwa, hususan kwenye  magonjwa kama malaria, Ukimwi na Kifua kikuu.Kuna upungufu wa Vituo vya afya 3913, vilivyopo ni 507 kati ya vituo 4,420 vinavyohitajika. (sawa na asilimia 11.5 ya mahitaji), Kuna upungufu wa Zahanati 8075, zilizopo ni 4,470 kati ya 12,545 zinazohitajika. (sawa na asilimia 35.6 ya mahitaji),”alisema

Mwakilishi wa TPSF, Samwel Nyantahe alisema serikali ya awamu ya tano imewezesha sekta binafsi kushiriki uchumi wa nchi na kuboresha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Mmoja wa wachangiaji katika mkutano huo, Luis Acaro kutoka TPSF alisema mkutano huo utawezesha sekta binafsi kutoa mawazo yao kwa serikali kwa kuwa wana mambo mengi lakini watakayozungumza ni masuala mtambuka yanayohusiana na kodi.

Alitolea mfano kuwa Uganda inapokuwa katika hatua za bajeti zimekuwa zikihusisha sekta binafsi ambayo imekuwa ikishiriki kikamilifu maandalizi ya bajeti ya serikali. 

Habari Kubwa