Mapipa 20 sumu yadakwa mgodini

17Jul 2017
Idda Mushi
Nipashe
Mapipa 20 sumu yadakwa mgodini

BARAZA la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imefanya ukaguzi wa kushtukiza katika eneo mgodi wa Mgalai wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro linalofanya uchenjuaji wa dhahabu na kukamata mapipa 20 yenye kemikali za sumu.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele.

Aidha, kampuni hiyo ikidaiwa kufanya shughuli zake kinyume cha taratibu.

Timu ya wataalamu wa NEMC kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Mvomero walifika kwenye mgodi huo umbali wa takribani kilometa 130  kutoka makao makuu ya wilaya ya Mvomero jana mchana na kushuhudia shughuli mbalimbali zikiendelea katika mgodi huo huku michirizi ya zinazodaiwa kuwa ni kemikali za sumu zikiwa zinachuruzika kuelekea mto uliopo jirani unaotumiwa na wananchi wa Kata ya Pemba kwa shughuli za kibinadamu na maeneo mengine ya jirani.

Hata hivyo, wahusika wa mgodi huo walikataa kutoa ushirikiano kwa timu hiyo, lakini baada ya askari polisi waliokuwa wameongozana na wajumbe hao kutishia kutumia nguvu ndipo waliokuwa mgodini hapo wakaruhusu ukaguzi ufanyike.

Meneja wa Ofisi ya Mkemia Mkuu Kanda ya Kati, Dodoa, Mussa Kuzumila, alisema katika ukaguzi huo walibaini makosa kadhaa likiwamo kumilikiwa kwa mapipa zaidi ya 20 yenye kemikali za sumu ambayo ni hatari kwa maisha ya viumbe hai na rekodi zimeonyesha yalishaingizwa mapipa 83 ya sumu hiyo mgodini hapo.

“Sumu hii ni hatari sana kama binadamu au kiumbe hai atavuta vumbi lake, itakuwaje ikitawanyika na kuwafikia wananchi kwenye makazi yao?” Alihoji Kuzumila.

Wakati ukaguzi huo ukiendelea alipatikana kijana mmoja aliyedaiwa kuwa raia wa Zambia, aliyejitambulisha kama mkemia wa mgodi huo, lakini hakuonyesha vitambulisho wala nyaraka zozote za kumruhusu kuishi au kufanya kazi nchini.

Baada ya kubanwa na ujumbe huo, kijana huyo alidai nyaraka zake zilichukuliwa na mwajiri wake, jambo lililoelezwa na maofisa hao kuwa ni kinyume cha taratibu.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka NEMC, Bernad Kongola, alisema kampuni hiyo inaendesha shughuli zake kinyume cha taratibu licha ya kupewa zuio na Mkuu wa wilaya ya Mvomero, ofisi ya mazingira wilaya na ofisi ya madini mkoa, lakini walikiuka na kuendelea na shughuli zao hivyo watawachukulia hatua za kisheria, ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Mmoja wa aliyejitambulisha kama mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji wa madini katika eneo hilo, Ibrahim Hozeni, alikanusha kuingiza kemikali hizo za sumu mgodini hapo, badala yake alidai kuingia mkataba na mwekezaji  mwingine na kwamba alishatoa taarifa polisi kuhusu ujio wa kemikali hizo, hivyo anashangaa na yeye kukamatwa na kushikiliwa kama mhalifu.

“Nilianza uchimbaji katika eneo hili tangu mwezi wa tisa mwaka jana, na nimekuwa nafanya uchimbaji mdogo kwa kutumia zana ndogo bila kutumia kemikali, lakini baada ya kuingia mkataba na mwekezaji nilijitoa na kumwachia majukumu ya kuendesha mgodi na mimi huwa napitia tu kukagua kinachoendelea na ndipo nilikutana na kemikali hizo na kuamua kutoa taarifa,” alijitetea Hozeni.

Wakati ukaguzi ukiendelea mtu mmoja  alipiga simu na kutaka kuzungumza na wakili wa NEMC na alijitambulisha kwa jina la Happyness William  akidai alikuwa mwekezaji wa  kampuni hiyo na inadaiwa pia ni kiongozi wa juu wa Serikali katika wilaya moja ya mkoa wa Pwani.

Alidai wamefuata taratibu zote, ingawa kulikuwa na ucheleweshwaji kwa baadhi ya maeneo hali iliyochelewesha utaratibu wa vibali na kuamua kuendelea na uzalishaji.

Kuhusu uhalali wa raia wa kigeni anayetumika kama mkemia katika kampuni hiyo, mwekezaji huyo alidai wameingia ubia na kampuni nyingine ya uchenjuaji ya Watanzania ya mkoani Mwanza na ndio wanahusika na ujio, ajira na malipo ya raia huyo.

Kutokana na maelezo hayo, Wakili Kongola akamtaka afike kituo cha polisi kwa maelekezo zaidi, lakini mtu huyo alikata simu.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambaye pia ni Ofisa Mazingira wa wilaya ya Mvomero, Msangi Ramadhani, alisema watu hao wamefanya ukaidi kwa muda mrefu kwani walikuwa wakipuuzia kila makatazo wanayopelekewa, hivyo kwa kuchukuliwa hatua utakua mfano kwa watu wengine.

Baada ya kukamilika kwa ukaguzi, NEMC kupitia Wakili Kongola iliagiza kufungwa mara moja kwa mgodi huo na watu watatu, akiwamo Ibrahim Hozeni, msimamizi wa mgodi huo Nurdini Hozeni na mkemia ambaye anadaiwa ni raia wa kigeni, Kelvin Malkom Kahonde walitiwa mbaroni sambamba na baadhi ya vifaa huku polisi wakiagizwa kuimarisha ulizi katika maeneo hayo.
 

Habari Kubwa