Maofisa maliasili waangua kilio baada kuachiwa huru mahakamani

21Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Maofisa maliasili waangua kilio baada kuachiwa huru mahakamani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imewaachia huru Maafisa wa Maliasili wanne baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa 58 waliyokuwa wakikabiliana nayo huku baadhi yao wakiangua kilio kwa furaha.

Walioachiwa huru ni Cheyo Mayunga ambaye ni Afisa Maliasili Mkoa wa Kigoma, Leonard Nzila ambaye (Afisa Maliasili Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Kaondime Mrangi ambaye ni Katibu Mhutas (PS) wa ofisi ya Maliasili na Hasheri Petro ambaye ni Wakala Mistu Mkoa wa Kigoma.

Maofisa hao walishtakiwa kwa makosa 58 ya kutumia nyaraka ya kumpotosha mwajiri, matumizi mabaya ya mamlaka pamoja na kusababishia serikali hasara ya Sh milioni 193 kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Hakimu wa mahakama hiyo Elia Baha, akitoa hukumu hiyo leo alisema
hakuna shahidi yeyote aliyeweza kuthibitisha kama washtakiwa walitenda makosa hayo na hivyo mahakama imeamua kuwaachia huru.

Washtakiwa baada ya kuachiwa huru mshtakiwa mmoja Cheyo Mayunga ambaye ni Afisa Maliasili Mkoa wa Kigoma aliangua kilio kwa furaha huku akipongezwa na ndugu zake waliofika mahakamani.

Kesi hiyo ya namba 1/2016 ilikuwa na mvuto watu wakiwemo ndugu za washtakiwa wafanyakazi wa maliasili pamoja na wananchi ambao walifika mahakamani kushuhudia kesi hiyo.

Habari Kubwa