Malipo hewa yabainika Muhimbili

16Apr 2017
Sanula Athanas
Nipashe Jumapili
Malipo hewa yabainika Muhimbili

Bidhaa zenye thamani ya Sh. milioni 450.57 ambazo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilizinunua katika mwaka wa fedha wa 2015/16 hazikufikishwa licha ya malipo kufanyika.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, kwa mashirika ya umma mwaka 2016/16 inabainisha kuwa bidhaa hizo ni kati ya zile za gharama ya Sh. bilioni 2.29.

Katika ripoti hiyo, CAG, Prof. Mussa Asad anasema
MNH walilipa kiasi chote cha fedha, lakini imebainika kuwa bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 1.84 ndizo zimefika na kupokewa na hospitali hiyo hadi kufikia Juni 2016, na kuacha bidhaa zenye thamani ya Sh. milioni 450.57 zikiwa hazijafikishwa na MSD.

"Kutokufika kwa muda kwa vifaa vya matibabu kunasababisha usumbufu kwa hospitali katika utoaji wa huduma ya tiba. Menejimenti inashauriwa kuchunguza suala husika na kufanya usuluhishi wa taarifa na MSD na kufanya ufuatiliaji wa bidhaa ambazo hazijaletwa," anasema.

Wakati mambo yakiwa hivyo kwa MNH na MSD
Prof. Assad anasema amebaini Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulitoa mkopo wa Sh. bilioni 44.29 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya cha Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini mkopo huo haukuwa na mkataba wala uthibitisho wa udhamini kutoka serikalini.

Anasema kuwapo kwa mkataba kungesaidia kuweka wazi haki na wajibu wa kila upande katika mkopo huo na utaratibu wa riba na urejeshaji wa mkopo.

"Kukosekana kwa mkataba na uthibitisho wa udhamini wa serikali kunaweza kuusababishia mfuko kupoteza fedha za wanachama endapo mkopaji atashindwa kuwa mwaminifu, na itakuwa vigumu kupata haki mahakamani," anasema.

Prof. Assad anaishauri menejimenti ya NHIF kuhakikisha mkataba wa mkopo unaingiwa kati yake na mkopaji na pia kuhakikisha kunakuwa na uthibitisho wa udhamini kutoka serikalini.

CAG pia anasema amebaini NHIF ilisaini hati ya makubaliano (MoU) na Wizara ya Afya pamoja na iliyokuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiitaka serikali kutoa fedha kwa ajili ya kuendesha malengo ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambayo ilihusisha gharama za kawaida za uendeshaji mfuko.

Prof. Assad anasema kuwa hadi kufikia Juni 30, 2015, NHIF ilipaswa kuwa imerejeshewa na serikali Sh. bilioni 1.2 kutokana na gharama ilizotumia kwenye miradi ya CHF kama ilivyoainishwa kwenye hati ya makubaliano, lakini gharama hizo hazikurejeshwa.

"Kushindwa kwa serikali kuilipa NHIF kumeuongezea mfuko mzigo mkubwa wa kifedha na kusababisha kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na kushindwa kupanua wigo wa shughuli zake," anasema Prof. Assad.

CAG pia anaishauri menejimenti ya NHIF kuhakikisha inashughulikia changamoto ya kukosekana kwa hatimiliki za viwanja saba vyenye thamani ya Sh. milioni 550.71 ambavyo mfuko huo ulivinunua katika miaka ya fedha 2013/14 na 2014/15 katika mikoa ya Tabora, Simiyu, Geita, Kigoma, Singida, Lindi na Kigoma.

SHIRIKA LA POSTA
Prof. Assad anasema amebaini Shirika la Posta Tanzania (TPC) linakumbana na changamoto za aina mbalimbali ukiwamo ukosefu wa fedha kwa ajili ya shughuli za utendaji na madeni ya muda mrefu, mfano deni la Sh. bilioni 3.87 linaloidai serikali kuhusiana na malipo ya pensheni kwa wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika.

Anasema shirika linahitaji mapinduzi makubwa ya kimkakati likilenga watu, michakato, teknolojia na fedha. Anaishauri serikali kulirejeshea Sh. bilioni 3.87 zilizotumika kuwalipa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Prof. Assad pia anasema TPC ilishindwa kulipa Sh. bilioni 1.38 kwa Mamlaka ya Udhibiti Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikiwa ni mjumuisho wa madeni ya ada ya mwaka na mirabaha kwa mwaka wa Fedha 2015/16 pamoja na miaka iliyopita.

Anasema katika mwaka 2015/2016 Sh. milioni 286.8 hakikulipwa kama fedha ya mrabaha na Sh. milioni tisa kama fedha ya ada ya mwaka, Sh. bilioni 1.08 zinawakilisha madeni ya miaka iliyopita, jambo ambalo ni kinyume cha kifungu cha 157 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010 na Kanuni ya 28(1) mpaka (3) ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2011 ambavyo vinahitaji shirika kuhakikisha linalipa mrabaha na ada kila mwaka kwa TCRA.

Habari Kubwa