Majeruhi wahitaji CT Scan

19Dec 2017
Rose Jacob
Nipashe
Majeruhi wahitaji CT Scan

BAADHI ya majeruhi wa ajali iliyoua watu watano na kujeruhiwa 14 Jumamosi katika Mtaa wa Buhongwa hapa Jijini Mwanza wanahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina kwa kutumia mashine ya CT Scan kufuatia hali zao kuwa mbaya, imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Abel Makubi alisema baadhi ya majeruhi mingoni mwa 14 waliopokelewa wanahitaji uchunguzi wa kina ikiwemo kipimo cha CT Scan.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi alisema ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu watano.Ajali hiyo ilihusisha gari namba T107 BKK Toyota Coaster mali ya kampuni ya Auki wa Mwanza na lori aina ya Scania lenye namba T504 BZB na tela lenye namba T880 ASA.

Kamanda Msangi alisema marehemu watano na majeruhi 13 wote ni abiria wa Toyota Coaster na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi dogo hilo.

Alisema dereva huyo alijaribu kupita magari mengine ya mbele yake bila kuchukua tahadhari.

Alisema madereva wote wa magari hayo walikamatwa na kwamba watafikishwa mahakamani pindi uchunguzi ukikamilika.

 

Habari Kubwa