Mahakama yamwachia huru DC wa Nchemba

16Apr 2017
Ahmed Makongo
Nipashe Jumapili
Mahakama yamwachia huru DC wa Nchemba

MAHAKAMA ya wilaya ya Bunda mkoani Mara, juzi imemwachia huru Mkuu wa wilaya ya Nchemba, mkoani Dodoma, Simoni Odunga, aliyekuwa anashtakiwa kwa tuhuma ya makosa ya wizi wa kuaminiwa na kutoa lugha ya matusi kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi.

Mkuu wa wilaya ya Nchemba, Simoni Odunga,

Alikuwa anashtakiwa na Veroline Odiambo, mkazi wa kijiji cha Bukore wilayani Bunda na kesi hiyo ilianza kusikilizwa mahakamani hapo, mwaka jana.

Katika shtaka la wizi, alikuwa anakabiliwa na wizi wa kuaminiwa wa Euro 2,758 (zaidi Sh. mil. 5), pamoja na kosa la lugha ya matusi kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, chini ya kifungu namba 20 kidogo cha kwanza A na cha pili cha sheria ya makosa ya mtandao.

Mahakama hiyo imemwachia huru Mkuu huyo baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Jaqueline Rugemalila, alisema katika kesi hiyo, upande wa mashtaka umeshindwa kuleta ushahidi unaojitosheleza kwa ajili ya kumtia hatiani mshtakiwa huyo.

Alisema kila upande ulileta mashahidi wanne, na baada ya kusikiliza kesi hiyo, amebaini kuwa mshtakiwa hakutenda makosa hayo na hivyo mahakama hiyo imemwachia huru.

Alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuithibitishia mahakama hiyo mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na ujumbe wa simu, kwa kuwa namba ya simu inaonekana kwa aliyeutuma ujumbe huo, lakini aliyetumiwa haionekani.

Hakimu Rugemalila alisema kwa msingi huo ushahidi huo haujitoshelezi na hauwezi kumtia hatihani mshtakiwa.

Aidha, alisema kuhusu uwakala pia ushahidi huo haujitoshelezi kumtia mtuhumiwa mahakamani kwa sababu kilichogundulika ni kuwa walikuwa na uhusiano ya kimapenzi.

Awali akimsomea mashtaka yake, Mwendesha Mashtaka wa polisi Hamuza Mdogwa, alisema mtuhumiwa huyo, alifanya makosa hayo wakati akiwa wakala wa mlalamikaji huyo ambaye walisoma naye katika shule ya msingi Bukore.

Alisema mlalamikaji alimpatia mtuhumiwa fedha hizo, akiwa kama wakala wake, ili azipeleke katika shule hiyo kwa ajili ya matumizi mbalimbali, lakini badala yake hakufanya hivyo na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.

Alisema kuwa mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kufanya kosa hilo kati ya mwezi desemba mwaka 2014 na Novemba mwaka 2015.

Nje ya mahakama, Mkuu huyo alisema anaishukuru mahakama hiyo kwa kutenda haki, kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa ya kutengeneza, ikiwa na lengo la kumchafua na kumharibia sifa yake mbele ya familia na jamii.

Wakati huohuo, nje ya mahakama hiyo mwendesha mashtaka wa polisi katika kesi hiyo, Hamuza Mdogwa, alisema kuwa hawajaridhika na hukumu hiyo hivyo tayari wameshakata rufaa.

Habari Kubwa