Madaktari walipuliwa uhaba watumishi 

31Dec 2017
Gurian Adolf
Nipashe Jumapili
Madaktari walipuliwa uhaba watumishi 

MEYA wa Manispaa ya Sumbawanga, Justine Malisawa, ameibua tuhuma nzito dhidi ya madaktari kuwa wanawaandikia magonjwa wasiyo nayo baadhi ya watumishi ili wahame vituo vya kazi.

MEYA wa Manispaa ya Sumbawanga, Justine Malisawa.

Amesema hatua hiyo inachangia kutokuwapo mgawanyo mzuri wa watumishi kwenye vituo vya kazi, hivyo kuwataka madaktari hao kuacha tabia hiyo mara moja. 

Malisawa aliyabainisha hayo juzi alipokuwa akitoa salamu za mwaka mpya wa 2018 na kuuaga mwaka 2017 kupitia kituo  kimoja cha redio mjini Sumbawanga.

Alisema baadhi ya madaktari ambao si waaminifu, wamekuwa wakishawishiwa na watumishi ili wawaandikie kuwa wanasumbuliwa na magonjwa ambayo hayaruhusu kuishi katika mazingira fulani, kwa kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya vituo kukosa watumishi. 

Kwa mujibu wa Malisawa, halmashauri inapowapangia maeneo ya kazi watumishi wake, baadhi yao wanakimbilia kwa madaktari na kupewa vyeti vinavyoelekeza kuwa maeneo hayo si rafiki kwa afya zao, hivyo kumwondoa kwa kuzingatia ushauri wa daktari ambao pengine si wa kweli. 

"Ninamwomba sana Mungu awajalie magonjwa yale wanayoyatamani kutokana na kwenda kwa madaktari kughushi vyeti vikionyesha kuwa wanasumbuliwa na magonjwa hayo ili wasikae katika vituo walivyopangiwa," Alisema.

Meya huyo alisema watumishi wa sekta ya afya, hasa madaktari, wanapaswa kutambua kuwa watoto wa vijijini pia wanahitaji watumishi bora ili kupata huduma bora kwa kuwa watumishi wengi wamekuwa na visingizio wanapopangiwa maeneo ya pembeni ya mji au vijijini. 

Malisawa alisema watumishi wa serikali wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuisaidia serikali katika kuwapelekea wananchi huduma sawa bila kujali wako vijijini au mijini kwa kuwa wote ni Watanzania.

 

Habari Kubwa