Maajabu 10 ya juisi ya nyanya

26Nov 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Maajabu 10 ya juisi ya nyanya

JE, una tatizo la kukosa usingizi? Na kama ni mwanadada, je, unahitaji kuwa na ngozi yenye mwonekano wa kuvutia zaidi kama ilivyo kwa warembo wengine?

Kama majibu ya maswali hayo ni ‘ndiyo’, basi juisi ya tunda la nyanya inaweza kuwa na msaada mkubwa. Ni kwa sababu, kwa mujibu wa rejea mbalimbali kuhusu faida za nyanya, juisi ya zao hilo huwa na manufaa zaidi ya 10.

Baadhi ya faida hizo ni kusaidia kuwaongezea urembo wa ngozi walaji wakiwamo kina dada na pia kupatikana kwa usingizi mnono kwa wale wenye tatizo la kuukosa.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Mtaalam wa Lishe, Dk. Aman Assey, alisema juisi itokanayo na nyanya imesheheni virutubisho muhimu kwa afya na ndiyo chanzo cha kuwapo na faida zaidi ya 10 za kiafya.

Akifafanua, Dk. Assey alisema kuwa kwanza, juisi ya tunda hilo husaidia ngozi kuwa na mvuto na mwonekano mzuri, huku pia ikimuondolea mlaji hatari ya kupata magonjwa ya ngozi.

Alisema kuwa pili, wale wanaosumbuliwa na matatizo ya usingizi wanaweza kupata nafuu au suluhu ya tatizo hilo kwa kutumia juisi ya nyanya.

Tatu, Dk. Assey alisema juisi ya nyanya husaidia pia kuimarisha nywele, hasa zile nyepesi kwa kuzifanya kuwa nzito.
 
“Nyanya imejaaliwa kuwa na virutubisho vingi kama vitamin C, A na K, madini ya potassium, manganese,

Cromium… na pia vitamini B1 na B6,” alisema na kuongeza kuwa virutubisho vingine ni pamoja na madini chuma, shaba, vitamin B2 na B3, magnesium, folate, phosphorous, protini, tryptohan, folate na molybdenum.

Kwa sababu hiyo, Dk. Assey alitaja manufaa mengine ya nne kwa wanayopata watumiaji wa juisi ya nyanya; ambayo ni kuboresha mbegu za uzazi kwa wote, yaani wanawake na wanaume wenye umri unaoruhusu masuala hayo.

"Wanawake na wanaume, wote wakinywa juisi (ya nyanya) huwasaidia kupata viini lishe vya kuwaongezea virutubisho kwenye mbegu za kiume na mayai ya wanawake ambavyo mwishowe husaidia kuzaliwa mtoto asiye na matatizo,” alisema Dk. Assey wakati akitaja faida ya tano ya uwezekano wa kuzaliwa kwa vichanga vyenye afya bora zaidi kutokana na kina mama kutumia juisi ya nyanya.

Faida ya sita, ni kuimarisha afya ya mifupa ya watumiaji wa juisi ya nyanya na faida ya saba, ni kusaidia kupunguza mauimvu ya mwili.

“Maajabu mengine ya juisi ya nyanya ni kuifanya mifupa yako kuwa imara na kama una maumivu makali mwilini, juisi ya nyanya itakusaidia kuondoa maumivu hayo,” alisema Dk. Assey.

Pia mtaalam huyo alitaja faida ya nane ya juisi ya nyanya ni kusaidia kupunguza uzito uliopitiliza na faida ya tisa, ni kuweka sawa kiwango cha sukari kwenye damu ya mlaji wa juisi ya nyanya.

Aidha, faida ya 10 ya jusi ya nyanya ni kumpunguzia mlaji uwezekano wa kupata saratani mbalimbali zikiwamo za tezi dume na ya utumbo.

“Nyanya inasaidia kumwondoa mtu kwenye hatari ya kupata saratani mbalimbali kama ya tezi dume, saratani ya utumbo, saratani ya kizazi kwa wanawake, ya koo na mdomo na mapafu,” alisema.

Aidha, Dk. Assey alitaja faida nyingine nyingi za juisi ya nyanya kuwa ni pamoja na kuimarisha nguvu ya uoni wa macho, kuondoa vijisumu mwilini, kutokana na tunda hilo kuwa na kiini kiitwacho ‘lycopene’ na pia uwezo mkubwa wa nyanya katika kutengeneza seli nyekundu za damu ya mlaji ambazo ni muhimu katika kuuepusha mwili na maradhi mbalimbali.

MAHITAJI
Mtumiaji wa nyanya anatakiwa kuiosha kulingana na kiwango cha juisi anayotaka, kisha akate vipande vidogo na kuhakikisha kuwa haondoi maganda yake.

Alisema mtumiaji anapaswa kuweka maji kidogo na kuyachemsha ili nyanya zilainike kabla ya kusubiri zipoe na kuzisaga. Sukari kidogo inaweza pia kutumika kwa ajili ya kuongeza ladha na baada ya hapo, juisi huwa tayari kwa kuinywa.

Habari Kubwa