Lowassa sasa ajitosa sakata la vyeti ‘feki’

14May 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Lowassa sasa ajitosa sakata la vyeti ‘feki’

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amejitosa katika sakata la hatima ya watumishi waliokutwa na vyeti feki vya kielimu na taaluma kwa kuiomba serikali kuweka mbele ubinadamu kwa kuwapa mafao yao.

Lowassa alisema licha ya watumishi hao 9,932 kudaiwa kukutwa na kosa la kughushi vyeti ili kujipatia kazi, bado wanastahili mafao kwa jasho walilolitoa kwa kipindi chao chote cha kulitumikia taifa, baadhi wakiwa ni kwa miaka mingi na kwa uadilifu mkubwa.

Suala hilo la vyeti feki, ni miongoni mwa mambo takribani matano ambayo kiongozi huyo aliyazungumzia ofisini kwake, Mikocheni jijini Dar es Salaam, jana.

Masuala mengine aliyoyatolea maoni ni ajali ya basi la wanafunzi wa shule ya Lucky Vincent iliyoua watoto 32, dereva na walimu wawili jijini Arusha; maafa yatokanayo na mvua zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini; tishio la njaa na uhuru wa kutoa maoni kupitia mitandao ya kijamii.

Jingine lililopata nafasi ni kutofanyika kongamano la demokrasia na siasa za ushindani baada ya ukumbi wa Anatoglo, Mnazi Mmoja waliouomba na kukabidhiwa kuutumia, kukatazwa saa chache kabla ya kufanyika kwa kongamano hilo kutokana na kuelezwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kwamba itautumia kwa shughuli nyingine.

Akifafanua kuhusu ombi lake la kutaka waliokutwa na vyeti feki walipwe mafao, Lowassa ambaye alizungumza jana kwa kofia ya kuwa mwenyekiti wa kongamano lililokwama dakika za mwisho jana, alisema kuwafukuza wafanyakazi zaidi ya 9,000 kunatia hofu.

“Kwa mfano kuwafukuza wafanyakazi zaidi ya 9,000 kwa wakati mmoja na kunyimwa mshahara wa mwezi na mafao yao, hawa watu waende wapi? Waliacha nyumbani mke na watoto wadogo, leo anarudi nyumbani hana kazi, hana mshahara wa mwezi wala hana mafao,” alisema.

Alisema hatetei kosa walilofanya la kukutwa na vyeti feki, bali ameiomba serikali kuweka mbele ubinadamu kwa kuwapa mafao yao kwa sababu vijana na wazee walitumikia taifa kwa uadilifu na wapo waliodumu katika utumishi kwa miaka 20 hadi 40.

Pia alisema suala hilo litasababisha shule nyingi kukosa walimu na hivyo serikali ilishughulikie kwa umakini mkubwa.

Kuhusu kongamano, alisema haikuwa sawa kutofanyika kwa sababu lilikuwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania pamoja na kuzungumzia suala la demokrasia.

“Tunalaani kitendo cha kuminya demokrasia, nia yetu ilikuwa moja. Lakini hawa wenzetu watambue kuwa ipo siku nchi hii itatawaliwa na watu ambao sio wao,” alisema Lowassa, ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita aligombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kuhama kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliwakilisha pia muungano wa vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo ni pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD. Kuhusiana na ajali, alisema ingekuwa vizuri siku ya kuaga miili Arusha Rais angekuwapo jijini Arusha.

Siku hiyo Rais aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Alitolea mfano tukio la kupigwa risasi askari mmoja nchini Uingereza ambalo Malkia aliagiza azikwe kitaifa na yeye kuhudhuria.

Kuhusu mafuriko yaliyosababishwa na mvua, alisema serikali inapaswa kutoa pole na matumaini kwa wananchi walioathirika.

Aidha, aliitaka serikali kuchukua hatua kuhusu kupanda kwa bei ya chakula kama unga wa sembe ambao sasa bei yake inazidi ya mchele na maharage.

Lowassa aliwapongeza waandishi wa habari kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhabarisha jamii, ingawa aligusia pia changamoto iliyopo ya uhuru wa kutoa maoni kupitia mitandao ya kijamii.

Pia alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa CCM kutokana na vifo vya makada wake, kiongozi wa zamani wa nafasi mbalimbali, Paul Sozigwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Thabiti Mwambungu.

Habari Kubwa