Kishindo kuagwa miili ya polisi

16Apr 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Kishindo kuagwa miili ya polisi

NI kishindo cha aina yake! Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na vigogo kadhaa wa Jeshi la Polisi akiwamo IGP Ernest Mangu, walikutana katika kikao maalumu jana katika kile kilichoonekana kuwa ni kupeana mikakati maalumu ya kukabiliana na uhalifu nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, akiwa na Naibu wake, Mhandisi Hamad Masauni, wakitoa heshima za mwisho mbele ya miili ya Askari nane, wakati wa shughuli ya kuagwa kwa askari hao kwenye viwanja vya Baracks jijini Dar es Salaam jana.

Kikao hicho cha aina yake kilifanyika ikiwa ni muda mfupi baada ya kuagwa kwa miili ya polisi wanane waliouawa Alhamisi wakati wakiwa kazini wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, shughuli iliyofanyika kwenye viwanja vya Polisi Kilwa Road jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji huku wengi wao wakilia mfululizo.

Aidha, Mwigulu na IGP Mangu walitangaza kiama cha aina yake dhidi ya wote walioshiriki kufanya unyama huo dhidi ya askari wasio na hatia.

Askari hao wanane waliuawa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi baada ya kuvamiwa ghafla wakati wakitoka eneo la kubadilishana lindo. Wauaji walishambulia gari lao aina ya Toyota Landcruiser wakati likiwa katika eneo la Mkengeni na kulishambulia kwa risasi kiasi cha kulifanya liache njia, kisha wakawafikia na kuwaua nane huku mmoja akijeruhiwa.

Askari hao waliouawa ni A/INSP Peter Kigugu mwenye miaka 38; F.3451 CPL Francis (34); F.6990 PC Haruna (34); G. 3247 PC Jacskon (29); H.1872 PC Zacharia (29); H.5503 PC Siwale (29); H. 7629 PC Maswi (24) na H. 7680 PC Ayoub mwenye miaka 23.

Akizungumza kabla ya kukamilika kwa shughuli ya kuagwa kwa miili ya askari hao jana, Waziri Mwigulu aliwataka viongozi wote wa wizara na jeshi la polisi waliofika eneo la tukio kutoondoka baada ya kuwaaga wenzao bali wabaki kwa ajili ya kufanya kikao maalumu cha kugawana majukumu.

“Tukimaliza hapa kuwaaga wenzetu, nawaomba viongozi tukae pembeni tugawane majukumu… hatuwezi kuruhusu uhalifu ukaendelea katika mazingira ya namna hii. Hatukubaliani kabisa na jambo hili,” alisema Mwigulu.

Waziri huyo aliongoza kuagwa kwa marehemu hao ambao walisafirishwa kwenda katika mikoa ya Morogoro na Lindi ambako awali marehemu walitoka kwenda Pwani kuongeza nguvu kwenye operesheni inayoendelea dhidi ya wahalifu. Shambulio hilo lilitokea Alhamisi saa 12:15 jioni, katika Kata ya Mjawa wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

ALIYONENA MWIGULU
Akizungumza mbele ya waombolezaji waliofurika kwenye viwanja vya Polisi Barracks Kilwa Road jana, Waziri Mwigulu alisema hakutakuwa na simile dhidi ya wahalifu waliotekeleza unyama huo.

“Ninawahakikishia Watanzania kuwa tuko katika kushughulikia masuala haya. Hiki kilichofanyika ndicho kinachotupeleka mbele kukabiliana na uhalifu wa namna hii,” alisema.

Mwigulu alisema jambo hilo linasikitisha na kwamba kitendo hicho kilichotendwa hakikufanyika kwa bahati mbaya bali kwa kupangwa na kwamba, suala hilo litashughulikiwa kwa ukamilifu ili kuhakikisha kuwa wahalifu wanashughulikiwa ipasavyo.

Akieleza zaidi, Mwigulu aliwataka wananchi kushirikiana kwa ukamilifu ili kuwezesha kukamatwa kwa wahalifu kwa sababu wamekuwa nao kwenye maeneo wanayoishi.

“Wananchi walio wema wajue kwamba serikali katika ahadi yake na viapo ya vijana tutawalinda, hawa waliofanya hivyo wakajificha kwenye nyasi wafikishieni taarifa kwamba hatutabakiza unyasi usimame,” aliongeza Mwigulu.

Aidha, Waziri huyo aliagiza wizara na jeshi la polisi kuacha tabia ya kuunda tume kwenye mambo ambayo hayahitaji taratibu hizo badala yake wanaoumia au kufa kazini wapewe haki zao mara moja.

IGP MANGU AONYA
Akizungumza katika shjughuli hiyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Mangu, alisema baada ya tukio hilo kutokea wapo baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuwakejeli polisi badala ya kuwapa pole na kuahidi kuwakamata mmoja baada ya mwingine.

“Nawaomba maofisa polisi na askari wenye vyeo mbalimbali, wanahabari, waombelezaji wapenda amani, watumie tukio hili kama changamoto. Tupeane nguvu siyo kukatishana tamaa.

“Kuna watu wameanza kutukejeli kwenye mitandao. Nikuhakikishie mheshimiwa Waziri kuwa tutawasaka watu hao,” alisema IGP Mangu.
Aidha, IGP Mangu alisema mashujaa hao wameuawa wakitekeleza majukumu halali na ya msingi kwa usalama wa nchi.

“Kuna watu ambao hawataki nchi ibaki kuwa na amani na kuamua kuvamia chombo kinachodumisha amani nchini, ila kama wana mpango wa kulikatisha tamaa jeshi la polisi wafute hilo kwa sababu wanatupa nguvu zaidi,” alisema.

Aliwataka wananchi kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa ili wahalifu wakamatwe.
“Tutaendelea kuchukua hatua mpaka tuhakikishe wanapatikana na wanashughulikiwa kama sheria inavyotaka.

Wananchi wa wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji wajue wahalifu wanazitumia wilaya hizi tatu kujificha kwenye nyumba zao. Tunaomba mtupe taarifa, mkishindwa kutupa taarifa itabidi tutumie nguvu kuzitafuta hizo taarifa ili tuwafikie hao wabaya wetu.”

Aidha, aliwataka makamanda wa mkoa wa Morogoro na Lindi watakapokamilisha mazishi hayo wakamilishe utaratibu wa malipo mara moja kwa wale watakaotakiwa kulipwa.

Habari Kubwa