Kisa TRA kumshushia rungu Askofu Kakobe

31Dec 2017
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Kisa TRA kumshushia rungu Askofu Kakobe

TUHUMA za kudaiwa kutoa kauli ya kujisifu kuwa fedha nyingi kuliko serikali ni miongoni mwa sababu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatilia kiundani mwenendo wa ulipaji kodi wa Askofu Zacharia Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) lililoko Mwenge, Dar es Salaam.

Askofu Zacharia Kakobe.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, ndiye aliyefichua siri hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Kuanzia juzi, sauti ya mtu anayedaiwa kuwa ni Askofu Kakobe imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikielezea mambo kadhaa ikiwamo madai ya mhusika kwamba ana fedha nyingi kuliko serikali na anao uwezo wa kumkopesha (fedha) waziri yeyote pindi akiombwa kufanya hivyo.

Akizungumzia hatua ya TRA kuchunguza ulipaji kodi wa Kakobe jana, Kamishna Mkuu  Kichere alisema licha ya kauli ya askofu huyo kuwa ana fedha nyingi kuliko serikali, rekodi zao zinaonyesha kuwa hajawahi kulipa kodi kama ilivyo kwa matajiri wengine nchini.

Kichere alisema wakiwa watu wa kodi, wamepokea kauli ya Kakobe kwa unyenyekevu mkubwa kwa sababu huwapenda watu wenye fedha nyingi ili wawape nafasi ya kulipa stahili yao.

“Kama mtu ana hela nyingi kuliko serikali… ambayo serikali yetu mnajua inatoa huduma, inanunua ndege, inajenga reli ya kati, barabara, elimu bure, inatoa mishahara kwa watumishi wa umma, inalipia madawa (dawa) hospitalini, inatoa huduma za usalama kwa wananchi, lakini serikali hiyo tunaambiwa imezidiwa fedha na Askofu Kakobe, basi ni jambo jema,” alisema Kichere

Aliongezea kuwa:”Kwa hiyo Askofu Kakobe ni tajiri sana kuliko serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa kuwa matajiri tunaowafahamu wanalipa kodi, basi baada ya kauli ya Askofu Kakobe ilibidi na sisi tupitie kumbukumbu zetu kuona jinsi tajiri sana anavyolipa kodi… utajiri unaendana na ulipaji kodi, nadhani wote mnalifahamu,” alisema Kichere kuwaambia waandishi wa habari.

Kamishna Kichere alisema pamoja na kusema  ana fedha nyingi kuliko serikali, ukweli ni kwamba TRA haina kumbukumbu ya ulipaji wowote wa kodi kwa Askofu Kakobe.

“Kuna watu ambao ni matajiri lakini hawaizidi serikali kwa fedha na tumeona wamekuwa wakilipa kodi. Kwenye kumbukumbu zetu, huyo tajiri Askofu Kakobe si miongoni mwao.

Hivyo sisi watu wa kodi tunataka tujiridhishe suala la kodi linalomhusu Askofu Kakobe na utajiri wake,’ alisema Kichere.

Aidha, alisema kwa kuwa wao ni wataalamu wa kodi, basi wana uhakika watafahamu kipato chake anachosema kinatokana na sadaka tu au kuna shughuli nyingine za kiuchumi ambazo Askofu Kakobe amekuwa akizifanya.

Alisema wanaelewa kwa mujibu wa sheria na taratibu, ni kwamba sadaka haitozwi kodi lakini wanafahamu kuwa taasisi za dini huwa zina shughuli zingine za kiuchumi,  hivyo  huenda Kakobe ana shughuli zingine za kiuchumi ambazo zinampatia fedha kiasi cha kuwa na fedha nyingi kuliko serikali.

“Lakini kama kweli ni sadaka peke yake ambayo inamfanya Askofu Kakobe awe na fedha nyingi kuliko serikali, ni jambo la kushtua kidogo, kwa sadaka tuu… basi sadaka ni nyingi kweli kweli.

Sisi ombi letu kwa Askofu Kakobe atoe ushirikiano kwa vijana wetu ambao watamtembelea kujiridhisha suala hilo.

“Kama kweli ana shughuli zingine za kiuchumi zinalipiwa kodi au la, pamoja na miamala mingine ili tuweze kujiridhisha kuhusiana na utajiri wake na ulipaji kodi wake,’ alisema

Aliongeza kuwa: ”Lakini kama ni sadaka peke yake, pia tutapata ukweli wake. Tuna utaalamu, tutajua kama ni sadaka peke yake au shughuli nyingine.

Atuambie tu kama ana shughuli za kiuchumi na akishatueleza tutapenda kujua hicho kipato kinalipiwa kodi au la…  hilo ndio la kwetu tunataka kujiridhisha kuhusiana na huo utajiri wake.”

Hivi karibuni, mbali na kudaiwa kutoa kauli kwamba ana fedha nyingi kuliko serikali, Kakobe alidaiwa kufuatiliwa na Jeshi la Polisi pia kutokana na tuhuma za uchochezi zinazohusiana na madai ya kuwatahadharisha wale wanaodhani kwamba taifa bado lipo kwenye mfumo wa chama kimoja.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema hawajawahi kumshikilia Kakobe na kwamba hilo litafanyika pindi ikionekana ipo haja ya kumkamata askofu huyo, umma utajulishwa.  

Habari Kubwa