JPM aongoza wakazi Dar kumuaga Ngwilizi

23May 2019
Romana Mallya
DAR
Nipashe
JPM aongoza wakazi Dar kumuaga Ngwilizi

RAIS John Magufuli amewaongoza waombolezaji kuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe, marehemu Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi, aliyefariki dunia Jumatatu ya wiki hii Hospitali ya Jeshi ya Lugalo alikokuwa akitibiwa.

Rais Dk. John Magufuli akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Brigedia Jenerali mstaafu Athuman Hassan Ngwilizi katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo, jijini Dar es Salaam jana. Marehemu alifariki dunia hospitalini hapo Mei 20, 2019. PICHA: IKULU

Mwili wa marehemu Brigedia Jenerali Ngwilizi aliagwa jana hospitalini hapo na baadaye alisafirishwa kuelekea Mlalo Lushoto mkoani Tanga kwa ajili ya mazishi.

Viongozi wengine walihudhuria shughuli hiyo ni  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo na Sheikh  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Mussa Salum.

Baada ya Rais Magufuli kuwasili hospitali ya Lugalo jana asubuhi alikwenda moja kwa moja kwenye eneo maalum lililowekwa kitabu maalum cha waombolezaji na kuandika.

Baada ya hapo alipita mbele ya jeneza la mwili wa Brigedia Jenerali Ngwilizi kutoa heshima zake za mwisho na kisha aliwapa pole familia ya marehemu.

Shughuli ya kuaga ilipokamilika wakati mwili ukiwa umebebwa na wanajeshi kuelekea kwenye gari maalum, Rais Magufuli aliambatana na viongozi wengine, ndugu, jamaa na marafiki kuusindikiza kutoka katika Hospitali ya Lugalo tayari kwa safari.

Katika uhai wake, Ngwilizi alitumikia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuanzia mwaka 1968 hadi 1993 katika nafasi mbalimbali hadi Brigedia Jenerali.

Pia, aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mbunge wa Kuteuliwa na baadaye Mbunge wa Mlalo, Lushoto mkoani Tanga kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015. Ndani ya Bunge aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Pia Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa Julai 2, mwaka huo, kuchunguza kashfa iliyomhusisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na Nishati, Eliakim Maswi, akiwatuhumu baadhi ya wabunge kula rushwa kutoka kwenye kampuni ya mafuta.

Kadhalika, aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -Tamisemi) wakati wa uongozi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Habari Kubwa