JPM akataa sifa akizindua hospitali ya Kimataifa Dar

26Nov 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
JPM akataa sifa akizindua hospitali ya Kimataifa Dar

KATIKA kuzingatia msemo wake kuwa siku zote msema kweli ni mpenzi wa Mungu-

Rais John Magufuli alikataa kupokea sifa kemkem alizopewa kuhusiana na ufanikishaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Kisasa ya Mloganzila na kusisitiza kuwa anayestahili pongezi hizo ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Rais Magufuli, ambaye ni maarufu pia kama JPM, alisema kuwa kamwe hayuko tayari kupokea sifa alizopewa kwa sababu wazo la mradi huo na hadi kuanza kwa utekelezaji wake, yeye alikuwa waziri tu na mwasisi wake ni Kikwete na hivyo, sifa zote anastahili rais huyo aliyemtangulia.

“Namshukuru sana Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa kuridhia kujengwa kwa hospitali hii. Bila yeye hii hospitali isingekuwapo leo hii. Ingawa watu wanapenda kusifiwa, lakini niseme ukweli hizi sifa siyo zangu… ni za Kikwete,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa na mamia ya watu waliokuwapo kushuhudia hafla hiyo ya uzinduzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila, ambayo pia ina hadhi ya kuwa ya rufani ya taifa kama Muhimbili.

Miongoni mwa wale waliokuwa wakimmiminia sifa Rais Magufuli kabla mwenyewe kuzikataa na kusisitiza kuwa zimuendee Kikwete ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na pia Waziri wa Elimu, Sayansia na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.

Wakizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli, mawaziri Mwalimu na Ndalichako walimpongeza Magufuli kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la kisasa hospitalini hapo lililogharimu Sh. bilioni 206.7, ambalo litakuwa linatumiwa kwa ajili ya kutoa tiba, kufundishia na kufanya tafiti za matibabu.

Akifafanua kwa kina sababu za kukataa sifa alizomwagiwa, Rais Magufuli alisisitiza kuwa kuanzia wazo la mradi huo na pia harakati za ujenzi wake, yeye alikuwa ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na hivyo alikuwa akitekeleza kile alichokuwa akiagizwa na Rais Kikwete kuhusu ujenzi wa hospitali ya kisasa.

“Aliniagiza nitafute eneo la kujenga hospitali na wakati natafuta, akanipigia simu…akaniambia nenda eneo la Mloganzila ambako kuna eneo la serikali. Sasa sifa kama hizi apewe mheshimiwa Kikwete,” alisema.

Akieleza zaidi, Rais Magufuli alisema alikuta eneo likiwa na ukubwa wa hekari 3,865.6, ambalo aliagizwa na Rais mstaafu Kikwete kuwa lote litumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Alisema eneo hilo lilikuwa katikati ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani na kwa sababu lilikuwa limevamiwa na baadhi ya wananchi, aliagizwa na Kikwete kuwa walipwe fidia wale walioendeleza viwanja vyao na mwishowe kuanza shughuli za ujenzi.

“Nimeona nizungumze haya ili msianze kumpa sifa mtu mwingine ambaye alikuwa anaagizwa tu. Muagizaji ndiye anatakiwa kupewa sifa. Na mimi nasema kwa dhati, msema kweli ni mpenzi wa Mungu… hizi sifa ni za Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na si zangu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema baada ya kuhamishwa wizara hiyo na kuwa Waziri wa Ujenzi, pia aliagizwa tena na Kikwete kujenga barabara ya kuelekea katika hospitali hiyo ya Mloganzila.

“Mimi nilikuwa naagizwa, haikuwa mamlaka yangu. Aliyekuwa ananiagiza ndiye anatakiwa kupewa sifa hizi za hospitali hii ya Mloganzila. Najua watu wanapenda sana kupewa sifa lakini hizi sifa si zangu… ni za Rais mstaafu  Jakaya Kikwete,” alisisitiza Rais Magufuli na kushangiliwa.

Aidha, Rais Magufuli aliisifia hospitali hiyo kuwa ni ya kimataifa na haijawahi kujengwa hapa nchini kwa sababu ina vifaa vya kisasa vya kutolea matibabu na kufundishia. Pia watoa huduma watakaoanza kutumia hospitali hiyo wamepatiwa mafunzo na Wakorea ambao ndiyo wameijenga.

MALENGO YA HOSPITALI
Rais Magufuli alisema malengo ya kujengwa kwa hospitali hiyo yalikuwa ni kufundisha wataalamu wa masuala ya afya kuanzia ngazi ya stashahada, shahada, shahada za uzamili na hadi uzamivu.

Alisema lengo lingine ni kutibu magonjwa mbalimbali na kufanya tafiti kuhusu namna ya kuboresha tiba na huduma za kinga.

Alisema serikali imeshatenga Sh. bilioni 13.32 kwa ajili ya kuanza kujenga miundombinu thabiti ya kufundishia, kumbi za
mihadhara na bwalo la chakula.

Alisema fedha hizo tayari zimeshakabidhiwa kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kwa ajili ya kuanza ujenzi huo ili kukamilisha lengo la hospitali hiyo la kudahili wanafunzi 15,000 na kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi wa afya nchini.

MAFANIKIO SEKTA YA AFYA
Rais Magufuli alisema katika kuhakikisha wanaboresha sekta ya afya, serikali ya awamu ya tano imejenga vituo vya afya vipya 268 na hivyo idadi ya jumla ya vituo hivyo nchini kufikia 7,284.

Kadhalika alisema serikali imetenga Sh. bilioni 171.9 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa vituo vya afya 760.

Rais Magufuli alisema pia serikali ina lengo la kuhakikisha inapunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kati ya vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 292 kati ya vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020.

Pia alisema nyumba 220 za watumishi wa afya zimejengwa na kuongezwa kwa bajeti ya vifaa tiba na dawa kutoka Sh. bilioni 31 hadi Sh. bilioni 269.

Habari Kubwa