JPM abariki kiama vigogo vyeti ‘feki’

16Apr 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
JPM abariki kiama vigogo vyeti ‘feki’
  • *Asema hadi sasa wamenaswa ‘vilaza’ 9,000

HATIMAYE ile kazi nzito ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma ili kutambua sifa zao za kielimu na kitaaluma inaelekea kuhitimishwa baada ya Rais John Magufuli kufichua kuwa tayari wameshanaswa 9,000 waliokutwa na vyeti feki na hivyo wako mbioni kushughulikiwa.

Rais John Magufuli, akikagua baadhi ya mabweni baada ya kuzindua majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam eneo la Mlimani jijini Dar es salaam jana.

Aidha, Nipashe imejulishwa kupitia vyanzo vyake kuwa miongoni mwa walionaswa na uhakiki huo na hivyo kuwa mbioni kuenguliwa kwa nafasi walizo nazo serikalini, ni pamoja na vigogo walioko kwenye idara na taasisi mbalimbali za serikali.

Akizindua mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jijini Dar Salaam jana, ambayo yamejengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 10 na Walaka wa Majengo nchini (TBA), Rais Magufuli alisema anasubiri ripoti atakayopelekewa ya wafanyakazi wa serikali wenye vyeti vya kughushi ili hatua zaidi zichukuliwe.

“Wafanyakazi waliofoji vyeti ni takribani 9,000. Naisubiri hiyo ripoti ije kwangu niifanyie kazi. Kwa hiyo mnaweza kuona shida zilizopo kwenye nchi yetu,” alisema Rais Magufuli maarufu kama JPM kuelezea changamoto alizokutana nazo tangu serikali yake iingie madarakani na kuongeza:

“Huku wafanyakazi hewa 19,000, mikopo hewa na wanafunzi hewa ambao waliokuwa ni 56,000.” Alisema sekta ya umma inakabiliwa na changamoto nyingi na hivyo yeye na serikali yake wanatakiwa kuzifanyia kazi.

“Kila mahali ninapokwenda kuna matatizo na lazima tuyakabili haya matatizo… kusingekuwa na matatizo msingenichagua. Mimi mliona ninaweza kuyakabili haya matatizo na ndiyo ninachokifanya sasa hivi,” alisema JPM.

Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kabla ya kauli ya JPM jana kuwa baadhi ya watumishi wa umma walishaanza kujiengua wenyewe serikali kwa visingizio mbalimbali, lakini kubwa ni baada ya kujua kuwa arobaini yao imefika baada ya serikali ya awamu ya tano kutekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kupambana na watumishi ‘vilaza’, wenye kutumia vyeti bandia ili kujipatia ajira.

“Kuna baadhi ya watumishi wanaoshika nafasi muhimu tayari wamejiengua kimyakimya baada ya kujua kuwa uhakiki wa vyeti hautawaacha salama,” chanzo kiliiambia Nipashe kabla Rais Magufuli kufichua jana idadi ya wenye vyeti feki kuwa ni watumishi 9,000.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi, Dk. Laurian Ndumbalo, aliiambia Nipashe katikati ya wiki kuwa wiki ijayo watatoa taarifa kamili kuhusu uhakiki wa vyeti vya watumishi.

MATUMIZI KUFURU, NJAMA TCU
Pia Rais Magufuli alisema, anafanya kazi ya kubana matumizi kwa sababu wapo watu waliokuwa wanafanya kufuru na ndio sababu ameamua kufunga makufuli ya kufuru.

Alieleza pia njama mbaya za baadhi ya watumishi wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ya kuwapangia wanafunzi katika vyuo vya watu binafsi na kuviacha vya umma.
Kufuatia wasiwasi huo, Rais Magufuli aliagiza TCU kuwapangia wanafunzi vyuo walivyochagua wenyewe.

Alisema kuwapo kwa utaratibu wa TCU kuwapangia wanafunzi vyuo kunasababisha vyuo vya serikali kama UDSM, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kukosa wanafunzi wa kutosha licha ya kuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi wengi.

HOSTELI YA KISASA, BEI POA
Rais Magufuli , pia alimuagiza Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandara, kuwatoza wanafunzi watakaoishi kwenye nyumba hizo, Sh. 500 kwa siku badala ya Sh. 800 inayotozwa katika nyumba nyingine za chuo, kiasi ambacho ni sawa na Sh. 15,000 kwa mwezi.

“Wanafunzi hawa wanalipa Sh. 800 lakini sijui nani aliyeyajenga hayo mabweni, lakini haya niliyojenga mimi tuwatoze Sh. 500 ili hela zinazobaki wanunue kalamu,” alisema Rais Magufuli na kuibua shangwe kwa wanafunzi waliokuwapo.

Kuhusu mikopo alisema mwaka juzi serikali ilitoa mikopo kwa wanafunzi 98,300, na mwaka huu serikali imetoa Sh. bilioni 483 ambazo zilitosha kwa wanafunzi 124,711 ingawa anaamini siyo wote waliopata walistahili.

Rais Magufuli alikumbushia pia mkasa wa wanafunzi wa kike kulazimika kuolewa ili wapate malazi na wanafunzi wa kiume kuoa kabla ya wakati.

“Ndio maana nilipoona kuna shida ya malazi hapa nikaamua kutoa ahadi ya kutafuta Sh. bilioni 10 ili kuhakikisha tunajenga nyumba za makazi ya wanafunzi hawa. Nilipokuwa nikazungumza ndugu zangu siku na uhakika kwamba hiki ninachokisema kitafanikiwa lakini nilimtanguliza Mungu,” alisema.

Alieleza zaidi kuwa awali alielezwa kuwa zinahitajika Sh. bilioni 150 hadi 170 kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo, lakini baada ya kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majengo (TBA), alimuahidi kufanya kazi hiyo kwa Sh. bilioni 10 tu na ndicho kilichofanyika.

Rais Magufuli alisema hosteli za Mabibo zilijengwa mwaka 2000 na ziligharibu Sh. bilioni 27 na zinachukua wanafunzi 4,000.

“Hizo zilijengwa miaka 10 iliyopita ziligharimu Sh. bilioni 27 lakini hizi zimejengwa leo kwa gharama za Sh. bilioni 10,” alisema.

Rais Magufuli, aliwashukuia viongozi na watendaji wa serikali ambao wamezoea kula asilimia 10 ya tenda za serikali na hivyo kuwanyima kazi wakandarasi wa ndani kuwataka kuacha mchezo huo mara moja.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza kuwa, wanafunzi wa UDSM ambao wanasomea masomo ya tiba kuhakikisha wanahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili, ambacho kimejengwa eneo la Mloganzila, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

AHOJI MAGARI YA CHUO
Kadhalika, Rais Magufuli, alihoji kutoweka kwa mabasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo yalikuwapo miaka ya nyuma.

“Niuombe uongozi wa Chuo, ebu angalieni utaratibu wa kuangalia uwezekano wa kununua mabasi hata matano ili kuwarahisishia huduma wanafunzi,” alisema.

Aidha, Rais Magufuli alimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitilya Mkumbo kwa weledi wake na kusema kuwa anaamini changamoto za maji katika chuo hicho atazitafutia ufumbuzi.

Kabla ya kuteuliwa na JPM, Kitilya alikuwa mshauri wa wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kabla ya kutangaza kuachana na siasa kwa asilimia 100 baada ya kuteuliwa na JPM.

Awali Waziri wa Elimu, Sayansi na Tenkolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alimshukuru Rais Magufuli kwa kuruhusu ujenzi huo wa mabweni na kuahidi kuwa sekta ya elimu itaendelea kuimarika, hasa kwa kutoa fursa kwa watoto wasiyo na uwezo kiuchumi kupata elimu bora na bure.

Habari Kubwa