Jela miaka 20 

20Dec 2017
Hellen Mwango
Nipashe
Jela miaka 20 

EMMANUEL Richard, dereva maarufu kwa jina la Humbe (30), jana alihukumiwa kwenda jela miaka 20 na kulipa faini ya Sh. milioni 32.7 baada ya kukutwa na hatia ya kupatikana na nyara za serikali, ikiwamo vipande vitano vya meno ya kiboko.

Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Muhini aliyesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa Jamhuri.

Alisema bila kuacha shaka, mahakama imemwona Humbe ana hatia.

"Mahakama hii imekuona una hatia, inakuhukumu kwenda jela miaka 20 na kulipa faini ya Sh. 32,750,000 kwa kosa la kukutwa na vipande vya meno ya kiboko," alisema Hakimu Muhini.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Septemba 12, 2016 eneo la Machinga Complex, lililopo wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na nyara hizo za serikali bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Ilidaiwa kuwa nyara hizo zina thamani ya dola za Marekani 1,500 (Sh. 3,277,500) mali ya serikali ya Tanzania.Mshtakiwa aliposomewa shtaka hilo alikana.

Habari Kubwa