Ilani ya CCM yatumbua wenyeviti

28Dec 2017
Daniel Limbe
Nipashe
Ilani ya CCM yatumbua wenyeviti

SIKU chache baada ya kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, kuwataka viongozi wa Chama hicho kuwawajibisha viongozi wa umma wanaokiuka utekelezaji wa Ilani ya CCM, baadhi ya wenyeviti wa vijiji wa chama hicho wilayani Sengerema wamejiuzulu nyadhifa zao.

Uamuzi huo wameufikia kutokana na malumbano ya kisiasa ya mara kwa mara ndani ya Chama hicho huku baadhi ya viongozi ngazi ya matawi wakichukua uamuzi mgumu kwa viongozi hao.

Waliojiuzulu ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Luchili (CCM), Ibrahimu Mbata na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamabano Kata ya Nyanzenda (CCM), Chuma Siyanyilila.

Mbata alisema ameachia ngazi kutokana na uongozi wa CCM tawi la Luchili kumwandikia barua ya kumsimamisha  wadhifa huo baada ya kumtuhumu kushindwa kusimamia shughuli za maendeleo.

Baadhi ya sababu zilizoainishwa kwenye barua ya kumsimamisha ni kushindwa kusimamia ujenzi wa choo cha shule ya msingi pamoja na ujenzi wa choo cha zahanati ya Luchili.

Aidha Mbata alidai kuwa tuhuma hizo hazikuwa na ukweli na zilitengenezwa ili kumharibia heshima yake kwa jamii, hivyo ameamua kumwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda, akimtaarifu kujiuzulu.

“Niliingia madarakani mwaka 2015 na nimefanya mambo mengi, lakini yote hawayaoni...nimefanikisha ujenzi wa Shule ya Msingi Kidete na sasa wanafunzi wanasoma bila shida baada ya Shule ya Msingi Luchili kujaa, lakini hilo hawalioni,” alisema.

“Malumbano ya kisiasa kwa viongozi wa chama ngazi ya kijiji na kata kulazimisha watakavyo wao ndiyo yamesababisha mimi kujiuzulu na kuachana na siasa kwa kuwa hakuna faida ila nilichokiambulia ni malumbano yasiyo na faida,” alisema Mbata.

Naye Siyanyilila, alikiri kujiuzulu baada ya kuandikiwa barua na viongozi wa CCM tawi la Nyamabano kuwa naye ameshindwa kusimamia shughuli za maendeleo.

Katibu wa CCM tawi la Luchili, Frenk Buhilya, alithibitisha kumwandikia mwenyekiti huyo barua ya kumsimamisha baada ya kamati ya maadili na uongozi kukaa na kubaini ameshindwa kutekeleza Ilani ya CCM hasa katika miradi ya maendeleo ukiwamo ujenzi wa choo cha zahanati ya Luchili kilichotakiwa kujengwa matundu mawili kujengwa tundu moja pamoja na mabati saba katika zahanati ya kijiji kupotea.

Katibu wa CCM Wilaya ya Sengerema, Idd Mkowa, alithibitisha kupokea barua za wenyeviti hao kusimamishwa nyadhifa zao.

 

Habari Kubwa