Idadi wazee yapaa kwa kasi

17Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Idadi wazee yapaa kwa kasi

IDADI ya wazee wanaotegemea kupata msamaha wa malipo ya matibabu katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro inafikia 2,112 kiwango ambacho kimeelezwa kupaa kwa kasi.

Kutokana na kiwango hicho kutajwa kuwa cha kasi, Manispaa hiyo imelazimika kufungua madirisha 15 yatakayoshughulikia utoaji wa huduma kwa wazee hao katika vituo vyake vya afya.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Michael Mwandezi imeeleza kuwa kwa hali ilivyo sasa, wameanzisha kampeni maalumu ya kuhamasisha wananchi wake kujiunga na Mfuko wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ili waweze kupata huduma za afya kwa unafuu.

“Kwa mwaka huu tunakusudia kuandikisha wanachama wa Tika 12,424, lakini mpaka sasa wanachama 5,560 tu ndiyo walioandikishwa ambao ni sawa na asilimia 45,”alisema.

Wakati Manispaa hiyo ikitambua idadi hiyo ya wazee wanaohitaji msamaha wa gharama za matibabu, bado taifa lina deni kubwa la changamoto ya kukwama kwa miaka 14, sera ya taifa ya wazee ya mwaka 1999 ambayo haijapelekwa Bungeni kutungwa na kuwa Sheria.

Akizungumzia uamuzi huo wa Manispaa ya Moshi kutoa msamaha wa matibabu kwa wazee hao zaidi ya 2,000, mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Women Tears Limited, Doreen Kimbi alitoa pongezi, lakini akataka ifanyike kazi kubwa ya kuwatambua wengine waliosalia.

Doreen alisema “Changamoto kubwa kwa wazee ninayoiona katika maeneo mbalimbali ni kushindwa kufikia huduma za matibabu na kumudu gharama.

"Na kwa kuwa mpango huu ni endelevu, Manispaa ya Moshi izungumze pia na wadau kama sisi tutoe elimu na huduma ya uchunguzi bure kwa wazee.”

Habari Kubwa