Hofu yaisha uhakika fidia 

31Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Hofu yaisha uhakika fidia 

SERIKALI imewaondolea hofu wananchi wanaotakiwa kuondoka katika eneo la mgodi wa dhahabu wa North Mara, Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara  kuwa wale waliofanyiwa tathmini watalipwa fedha zao.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, alisema hayo juzi wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Nyabichune, Kata ya Matongo wilayani Tarime kwenye mkutano na wananchi na wachimbaji wadogo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo hayo walimweleza Naibu Waziri malalamiko mbalimbali ikiwamo ulipaji wa fidia, ajira, uhusiano duni na mgodi pamoja na mgodi kushindwa kununua bidhaa zinazozalishwa na wananchi wa maeneo hayo. 

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Nyongo aliuagiza mgodi huo wa North Mara kuhakikisha unawalipa wananchi fidia wanayostahili.

 “Haiwezekani mmefanya tathmini halafu baadaye mnageuka kwamba hamtalipa. Ubabaishaji wa aina hiyo haupo maana mlikuwa mmekwishawaandaa wananchi kisaikolojia kwamba mtawalipa,” alisema.

Pia aliwaonya wananchi wanaofanya udanganyifu kuacha tabia hiyo mara moja kwa kuwa kufanya hivyo kunasababisha malipo ya fidia kuchelewa kwa wale wanaostahili.

“Hapa nimeelezwa tathmini ya kwanza ilikuwa na kiasi kidogo cha fidia kilichokuwa kinadaiwa tofauti na tathmini ya mara ya pili. Hapa inaonekana kuna baadhi yenu wamefanya udanganyifu,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuwatambua waliofanya udanganyifu ili kuharakisha ulipaji wa fidia kwa mujibu wa sheria na makubaliano.

Kuhusu ajira, Nyongo aliuagiza mgodi huo kuhakikisha unatoa kipaumbele kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka mgodi na hapo hapo aliwaasa wananchi watakaonufaika na ajira hizo kufanya kazi kwa uadilifu.

“Ajira zitolewe kwa wenyeji wenye sifa na nyie ndugu zangu mkipewa kazi fanyeni kwa uadilifu, msiwaharibie wengine wenye nia ya kufanya kazi,” alisema Nyongo. 

Kwa upande wa bidhaa na huduma kutoka kwa wenyeji, Nyongo alisisitiza mgodi kutumia huduma na bidhaa zinazozalishwa na wenyeji jambo ambalo alisema likifanyika kwa weledi litachangia katika uboreshaji wa uhusiano baina ya pande hizo mbili.

Aidha, alitoa rai kwa Halmashauri kuwa fedha wanazopokea za ushuru wa huduma (service levy) kutoka mgodini hapo ambazo zinatakiwa kuleta maendeleo hapo Nyamongo zirudishwe hapo kufanya maendeleo. 

Habari Kubwa