HESLB kuwasaka wadaiwa sugu 119,497 

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
HESLB kuwasaka wadaiwa sugu 119,497 

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo nchini (HESLB), Abdul Razaq Badru, amesema kuanzia Januari 08 mwaka huu wanatarajia kuanza kuwasaka jumla ya wanufaika wa mikopo 119,497 kote nchini ambao wamekiuka sheria iliyoanzishwa na  bodi hiyo kwa kutoanza kurejesha mikopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo nchini (HESLB), Abdul Razaq Badru.

Aidha amesema kuanzia mwaka jana mpaka sasa wamefanikiwa kuwapata wadaiwa sugu 26,000 wa mikopo ya elimu ya Juu na bado wanaendelea na msako wa kuwatafuta wengine.

Badru amesema hayo leo Januari 3 wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake akielezea namna bodi yake ilivyojipanga kuendelea kuwakabili wadaiwa sugu kwa mwaka 2018.

Hata hivyo amewapongeza waajiri kwa kutoa ushirikiano wao kwa kuendelea kuwasilisha makato ya mishahara kwa waajiriwa wao wanaodaiwa na bodi hiyo kwa asilimia 15 kama sheria inavyoelekeza japo bado kuna waajiri ambao hawajatoa ushirikiano kwani bado hawajaanza kuwakata waajiriwa wao.

"Kuanzia Januari 8  mwaka huu tutaanza kufuatilia taarifa za waajiriwa katika taarifa zao za kibenki ili kubaini nani ni mnufaika wa mkopo ili kuanza kurudisha fedha hizo HESLB ili kuweza kuendelea kunufanisha wahitaji wengine", alisema Badru.

Mpaka sasa HESLB inadai jumla ya bilioni 285 kwa wadaiwa  wote, huku lengo la mwaka huu hadi kufikia Julai waweze kukusanya wastani wa madeni hayo kwa mwezi uwe umefika bilioni 17 kutoka bilioni 13 kama ilivyokuwa awali.

  

Habari Kubwa