Dereva wa ajali basi, Hiace iliyoua 7 kortini

03Jan 2018
Joctan Ngelly
Nipashe
Dereva wa ajali basi, Hiace iliyoua 7 kortini

Abubakari Hamisi (40), dereva wa basi na mkazi wa Ujiji ambaye anatuhumiwa kwa kugonga Hiace na kusababisha vifo vya watu 7 na majeruhi 11, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Kigoma kwa makosa 20.

Mshtakiwa huyo ameshtakiwa kwa makosa 20 ambapo makosa 7 ni kusababisha vifo, makosa 11 ni kusababisha majeruhi na makosa 2 ni kusababisha uharibifu wa magari yote mawili, kitendo ambacho Jamhuri inadai ni kinyume cha sheria.

 

Mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Fredrick Shayo na aliposomewa mashtaka yote 20, alikana na yuko nje kwa dhamana ya wadhamini wawili ambao waliwasilisha barua za ofisa mtendaji wa kata na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni 5 kwa kila mmoja.

 

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Raymond Kimbe, ulidai kuwa upelelezi umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali.

 

Hakimu Shayo alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali.

 

Akisoma hati ya mashtaka, Kimbe alidai kuwa Desemba 20, mwaka 2017 majira ya asubuhi katika Kijiji cha Kabeba Wilaya ya Uvinza katika barabara ya Ilagala-Kigoma mshtakiwa huyo alikuwa akiendesha gari namba za usajili T 383 BMG aina ya Scania bus ya Kampuni ya Saratoga, iligonga Hiace namba T 237 BCE na kusababisha vifo vya watu 7, majeruhi 11 na uharibifu wa magari yote mawili, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa