DC Ubungo ataka amani uchaguzi wa udiwani leo

26Nov 2017
Margaret Malisa
Nipashe Jumapili
DC Ubungo ataka amani uchaguzi wa udiwani leo

MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, amesisitiza umuhimu wa kuwapo kwa amani na utulivu katika uchaguzi wa marudio wa kumpata diwani wa Kata ya Saranga huku akionya kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vurugu.

MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori.

Makori alitoa onyo hilo mwishoni mwa wiki wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wasimamizi wa uchaguzi kwenye vituo vya kupigia kura ambapo pamoja na mambo mengine, aliwataka wakazi wa kata ya Saranga kujitokeza kupiga kura kwa utulivu na kujiepusha na vurugu za aina yoyote.

" Uchaguzi huu utafanyika kwa usalama wa kutosha katika vituo vyetu vyote vya kupigia kura… usalama ni muhimu ili kila mwananchi wa Kata ya Saranga atumie haki yake ya  kidemokrasia kupiga kura,” alisema Makori, huku akiwataka wasimamizi kufanya mambo yote kwa uwazi katika uchaguzi huo na kuwashirikisha mawakala wa vyama vya siasa kama sheria inavyoelekeza na hivyo kuepusha malalamiko yasiyo ya msingi.

Kwa mujibu Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Ubungo, Valence Urassa, kurudiwa kwa uchaguzi wa diwani kata ya Saranga leo kumetokana na uamuzi wa mahakama kutangua matokeo ya awali ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Harun Mdoe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiye aliyefungua kesi kupinga ushindi wa Ephraim Kinyafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mbali na uchaguzi huo wa katika kata ya Saranga, pia chaguzi nyingine za marudio zinafanyika katika kata 43 zilizopo kwenye
Halmashauri 36 nchini.

Vituo 884 vitahusika huku wapigakura 333,309 walioandikishwa katika daftari la kudumu la Wapigakura ndiyo wanaotarajiwa kushiriki.

Habari Kubwa