CWT Simanjiro yampa kongole JPM

13Jan 2018
John Ngunge
Nipashe
CWT Simanjiro yampa kongole JPM

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Simanjiro, kimempongeza Rais John Magufuli kwa kuagiza kutolewa kwa Sh. bilioni 200 ili kulipa madeni ya ndani yakiwamo ya walimu. 

Rais John Magufuli.

Mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa, Abraham Kisimbi, alisema hatua aliyochukua Rais Magufuli inastahili kupongezwa na walimu wote nchini. 

“Walimu wilayani hapa wamefarijika mno tangu Rais Magufuli alipotangaza kuwa Sh. bilioni 200 zitatumika kulipia madeni yakiwamo ya walimu nchini,” alisema. 

Alisema walimu wana imani kubwa na serikali yao kwamba inawajali.

"Mara baada ya kupata taarifa ya Rais Magufuli kutoa ahadi hiyo walimu wa wilayani hapa wameshukuru mno kwa kuwa mahitaji yao waliyokuwa wanatarajia yatafanikiwa muda siyo mrefu," alisema.

Alisema tangu tamko hilo lilipotamkwa na Rais Magufuli, walimu wanafanya kazi kwa furaha zaidi kwa kuwa walisubiri kwa muda mrefu kulipwa madeni yao.

Januari 2, mwaka huu, Rais Magufuli alisema, mwezi ujao serikali itatoa Sh. bilioni 200 kwa ajili ya kulipa madeni ya ndani yatakayokuwa yamehakikiwa yakiwamo ya wazabuni waliotoa huduma katika taasisi za serikali, madai ya walimu na madai ya wakandarasi.

Alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akiagana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliyemaliza muda wake, Profesa Benno Ndulu leo Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Gavana mpya wa benki hiyo ni Profesa Florens Luoga. 

Katibu wa CWT wilayani Simanjiro, Nazama Tarimo, alipongeza hatua ya Rais Magufuli kwa kudai kuwa imeongeza utendaji wa kazi.

Alisema walimu wa Wilaya ya Simanjiro, wana imani kubwa kuwa fedha zao zitapatikana hivi karibuni kwa kuwa ni muda mrefu walisubiri kulipwa madeni yao. 

“Limekuwa jambo zuri kwa walimu kuahidiwa kulipwa fedha zao na Rais Magufuli, bila kukwaruzwa na serikali wala kutangaziana kufanyika kwa migomo. 

"Walimu wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa ajili ya kuongeza tija na ufaulu wa wanafunzi ili haki yetu walimu iendane na wajibu," alisema.  

Habari Kubwa