CRB yashtukia matapeli wanaotumia jina lao

16Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
CRB yashtukia matapeli wanaotumia jina lao

BODI ya Usajili wa Wakandarasi Nchini (CRB), imewatahadharisha wananchi, watu  wenye miradi ya ujenzi pamoja na wakandarasi nchini kuwa makini na watu wanaotumia jina la bodi hiyo na kufanya utapeli.

Msajili wa bodi hiyo, Rhoben Nkori.

Msajili wa bodi hiyo, Rhoben Nkori, alisema kwenye taarifa yake kuwa bodi imewataka wananchi na wakandarasi wawe wanatoa taarifa katika ofisi za bodi za Makao Makuu Dar es Salaam na Kanda zake ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wa aina hiyo.

“CRB ina ofisi za kanda ambazo zinafanya kazi nchi nzima, kanda hizo ni Kanda ya mashariki – Dar es salaam, Kanda ya kaskazini  Arusha, Kanda ya kusini Mbeya,  Kanda ya ziwa Mwanza na Kanda ya kati  Dodoma, watumie ofisi hizi wasirubuniwe na matapeli,” alisema Nkori.

Aidha, alisema watumishi wa CRB wamekuwa wakienda kwenye ukaguzi wakiwa na vitambulisho vya bodi hiyo na vizibao vyenye nembo ya CRB vinavyowatambulisha kuwa wanatoka kwenye bodi hiyo.

Alisema kuna watu ambao wamekuwa wakijiita wawakilishi wa Bodi hiyo na kufanya shughuli za bodi hiyo kwa njia ya utapeli na kuchukua rushwa kwa wakandarasi na wenye miradi.

Alisema watu hao wamekuwa wakijitambulisha kama wawakilishi wa bodi hiyo ambao huwa wanakwenda kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi maeneo mbalimbali.

Alisema watu hao hutembelea sehemu zenye miradi na kuwatisha watu wanaofanya shughuli za ujenzi na kuwaomba rushwa ili wasiwashtaki wanapobaini kasoro kwenye miradi yao.

Aidha, alisema watu hao wamekuwa wakiwaandikia barua watu wenye miradi ya ujenzi wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua na bodi kwa kufanyakazi zao bila kuzingatia masharti ya ujenzi kama vile kuweka vibao vya kuonyesha mkandarasi anayejenga.

“Sisi CRB hatuwatambui watu hao na tunawaomba wananchi na watu wenye miradi ya ujenzi wawe makini na wakiwa na tatizo waende kwenye ofisi za kanda zetu ambazo tumezitaja kama kuna watu anahisi wanataka kumtapeli awasiliane na bodi ili tumkamate na kumfikisha mahakamani,” alisema

Gazeti hili lilifanikiwa kupata nakala ya barua yenye nembo ya CRB iliyoandikwa na mmoja wa matapeli hao kwenda kwa mmoja wa wateja akidai kutaka ufafanuzi wa baadhi ya mambo kwenye mradi wake wa ujenzi unaoendelea.

Habari Kubwa