Clouds washtukia jambo sakata Masoud Kipanya

03Jan 2018
Salome Kitomari
Nipashe
Clouds washtukia jambo sakata Masoud Kipanya

UONGOZI wa kampuni ya Clouds Media Group (CMG) umeonyesha kushtukia jambo kuhusiana na mtangazaji wake ambaye pia ni mchoraji wa katuni zinazoakisi masuala mbalimbali ya kijamii, Masoud Kipanya.

Masoud Kipanya.

Juzi, katika mitandao mbalimbali ya kijamii kulisambaa taarifa zilizodai kuwa Kipanya alitoweka na kwamba hapatikani kwenye simu yake ya mkononi iliyokuwa ikiita bila kupokewa na uvumi mwingine ulidai kuwa alikamatwa kwa tuhuma za uchochezi.

 

Hata hivyo, hakukuwa na taarifa za polisi kuthibitisha lolote kati ya tetesi hizo zilizosambaa haraka kupitia mitandao ya kijamii.

Baadaye, Kipanya kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter aliibuka na kuwashukuru waliosambaza ujumbe uliovumisha kukamatwa kwake akidai kuwa "umesaidia".

“Poleni kwa usumbufu na asanteni kwa kujali hali za wengine. Niko salama. Alhamdulillah. Namshukuru pia aliyesambaza taarifa. 'AMESAIDIA’," ulisomeka ujumbe huo na kuibua maswali mengi kuhusu neno hilo la 'amesaidia'.

Jana mchana, Nipashe ilimtafuta kwa simu Masoud ambaye baada ya kuombwa ufafanuzi wa ujumbe wake huo na ukweli kuhusu madai ya kukamatwa kwake, alisema hayuko katika nafasi nzuri na hivyo kuomba asizungumzie suala hilo kwa muda huo.

“Naomba nikupigie baadaye,” Masoud alimwambia mwandishi wa Nipashe.

Baadaye, simu yake ilikuwa inaita bila kupokewa na wakati mwingine kukatwa na hata alipotumiwa ujumbe wa kukumbushwa kuhusu ufafanuzi alioahidi, hakukuwa na majibu. 

TAARIFA YA CLOUDS

Katika taarifa yake kwa umma jana, uongozi wa Clouds ulieleza kuwa unawashukuru Watanzania kwa msaada wao katika suala linalomhusu mtangazaji wao huyo.

Aidha, katika maelezo yake zaidi kwenye taarifa hiyo, ndipo Clouds ilipogusia kile kinachoonyesha kwamba kuna hisia za kuwapo kuhusiana na sakata hilo la uvumi kuhusu Kipanya.

“CMG inatambua kuwa kilichohusishwa katika suala la Masoud Kipanya kinahusiana na ‘talanta’ yake ya ziada katika tasnia ya sanaa,” ilifafanua taarifa hiyo, ambayo uongozi wa CMG ulikiri kuitoa wakati ulipotafutwa na Nipashe jana.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa suala la Kipanya limejadiliwa na mamlaka husika, na sasa tayari anaendelea na shughuli zake nyingine za ujenzi wa taifa.

Hata hivyo, hakukuwa na maelezo ya kina zaidi kuhusiana na taarifa hiyo na jana, Kipanya alisikika akitangaza redioni kama kawaida.

Adha, alipotafutwa jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa naye amesikia tu kuhusu taarifa hizo za kuwahi kukamatwa kwa Kipanya na kwamba, wanafuatilia kwenye vituo mbalimbali vya polisi kujua ukweli wa kilichotokea.

Uvumi kuhusiana na taarifa za Kipanya uliibua mijadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii huku wengine wakielezea hofu yao kutokana na taarifa za hivi karibuni juu ya kutoonekana kwa siku zaidi ya 40 sasa kwa mwandishi wa Mwananchi, Azory…na pia kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaderma), Ben Saanane. Msanii wa bongofleva, Roma Mkatoliki, aliwahi pia kuripotiwa kupotea kabla ya kujitokeza hadharani siku chache baadaye.

 

 

Habari Kubwa