Chanzo kukamatwa Mbunge Katibu Mkuu Chadema ni hiki

16Jul 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Chanzo kukamatwa Mbunge Katibu Mkuu Chadema ni hiki

VIONGOZI sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji, na wabunge wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kwa madai ya kufanya mkutano bila kibali.

Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji.

Wabunge hao ni Cecil Mwambe wa Ndanda mkoani Mtwara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini na Zubeda Sakuru wa Viti Maalum mkoa wa Ruvuma.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi, Gamin Mushi, alitaja sababu za kukamatwa kwao kuwa ni kufanya maandamano na mkutano bila kibali.

Kamanda Mushi aliwataja wengine waliowakamata kuwa ni Katibu wa Ulinzi Taifa wa Chadema, Sanuda Manawa, Katibu Mwenezi Charles Makungara na Katibu wa Chadema Kanda ya Kusini, Silibeth Ngatunga.

Pia Kamanda Moshi alisema wanawashikilia watu hao kutokana na kukiuka maelekezo yaliyotolewa awali kuhusu kufanya mikutano.

“Mikutano ambayo inaruhusiwa ni ile inayohusisha viongozi kutoka eneo husika lakini si kiongozi wa taifa wa chama anakuja kwenye mkoa fulani kufanya mikutano,” alisema.

Aidha, alisema idadi ya watu hao inaweza kuongezeka kwa sababu Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka wote waliokuwapo kwenye mkutano huo.

“Wananchi wa Ruvuma endeleeni na shughuli zenu na tumezuia mikutano yote ambayo ilipangwa kufanyika kwenye mkoa huu kwa sasa,” alisema.

Awali, Ofisa Uhusiano wa chama hicho, Tumaini Makene, aliiambia Nipashe jana kuwa viongozi hao wanashikiliwa na Polisi wilayani Nyasa na kwa wakati huo (jioni) walipelekwa kituoni kuhojiwa.

Makene alisema Dk. Mashinji alitakiwa kueleza kwa nini yuko Mbamba Bay mkoani Ruvuma.

“Polisi wamemkamata Katibu Mkuu Dk. Mashinji, Mbunge Mwambe na Mbunge Zubeda baada ya kuvamia kikao cha ndani kilichokuwa kikiendelea mjini hapo ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu Dk. Mashinji kukagua shughuli za chama katika majimbo ya kanda hiyo iliyoanza leo (jana),” alisema.

Habari Kubwa