CCM Korogwe yapania kuwatimua wala rushwa

16Jul 2017
Dege Masoli
Nipashe Jumapili
CCM Korogwe yapania kuwatimua wala rushwa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Korogwe Mjini, kimetishia kuwatimua uanachama watu watakaokwenda kinyume cha taratibu za chama hicho katika uchaguzi bila kujali nafasi aliyonayo mtu, umaarufu wala uzoefu wake ndani ya chama hicho.

Akizungumza  katika mkutano maalumu wa baraza la wazazi  kujadili majina ya wagombea nafasi mbalimbali, Katibu wa CCM  Korogwe Mjini, Ally Issa,  alisisitiza suala la uadilifu na kwamba hakuna mtu atakayebebwa kutokana na umaarufu wake, cheo wala uzoefu wa siku nyingi ndani ya CCM ama Jumuiya zake, bali lililo muhimu kwa kila mmoja ni uadilifu na kuzingatia misingi ya chama chao.

Issa  alisema mchakato wa kuwapata watu wa kusimamia kura lazima ufanyike kwa umakini huku akiwataka wasimamizi hao wa kura kutenda haki  na kwamba  mtu  atakayekwenda kinyume atahesabika kama mwenye kutaka  kuua chama chao wilayani humo.

Alisisitiza kuwa miongoni mwa sifa muhimu kwa kila mmoja, ni kujiweka mbali na vitendo vya rushwa.

Akizungumzia zaidi uhai wa chama wilayani humo, katibu huyo alisema CCM haiko tayari kuona baadhi ya watu kuasisi makundi ambayo yamekuwa yakileta mgawanyiko miongoni mwa wanachama.

"Chama chetu hakina mtu mkubwa au mheshimiwa. Ndiyo maana tunatakiwa kuitana ndugu. Hivyo yeyote atakayekwenda Kinyume cha taratibu bila, kujali ni nani atafukuzwa," alisema Ally.

Hivi sasa, CCM na jumuiya zake ikiwamo ya Wazazi, iko katika mchakato wa kuchagua viongozi katika nafasi mbalimbali.

Habari Kubwa