CAG apingana na Ndalichako

16Apr 2017
Sanula Athanas
Nipashe Jumapili
CAG apingana na Ndalichako

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amesema kuchelewa kwa utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 53 za walimu ulio chini ya Mamlaka ya Elimu (TEA) umetokana na serikali kuchelewa kutoa pesa.

JOYCE NDALICHAKO

Katika ripoti yake ya mwaka 2015/16 iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 27 na kuwasilishwa bungeni mjini hapa Alhamisi iliyopita, CAG Assad anasema ukaguzi wake umebaini mradi huo uliotengewa Sh. bilioni 7.5 na kutakiwa kukamilika Juni 30, 2016, haujatekelezwa kikamilifu kutokana na serikali kutotoa pesa kwa wakati.

Ripoti hiyo inakinzana na maelezo ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako aliyoyatoa Machi 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwamba; tayari serikali ilishaipa TEA Sh. bilioni 29 kwa ajili ya mradi huo na mingine ya kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2015/16 lakini hazijatumika.

Prof. Ndalichako aliyasema hayo siku hiyo alipokuwa anazindua bodi mpya ya TEA aliyoipa miezi mitatu kuanzia siku hiyo kuhakikisha inatekeleza mradi huo wa ujenzi wa nyumba za walimu na mingine iliyoikuta.

Katika ripoti yake, CAG Assad anasema amebaini mwaka 2015/16, TEA ilipanga kujenga nyumba 53 za walimu katika sehemu mbalimbali zisizofikika kirahisi kwa gharama ya Sh. bilioni 7.5.

Hata hivyo, Prof. Assad anasema mamlaka hiyo ilifanikiwa kujenga nyumba 15 kwa kuchelewa kutokana na ujenzi kuanza Agosti 2016 hadi Desemba 2016).

"Kuchelewa kwa mradi huu kulisababishwa na serikali kuchelewesha kuwasilisha fungu la pesa zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu na mchakato wa kutafuta wazabuni wa ujenzi wa nyumba hizo," Prof. Assad anasema katika ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za mashirika ya umma.

Anaishauri serikali kuweka fungu la kutosha katika muda sahihi kwa mamlaka ili kukamilisha miradi yake na kuondoa tatizo la makazi ya kutosha kwa walimu.

Uhaba wa nyumba bora kwa ajili ya walimu nchini ni moja ya changamoto ambazo zinatarajiwa kuwa 'mwiba' kwa Waziri Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene kipindi hiki cha mkutano wa Bunge la Bajeti mjini hapa.

Habari Kubwa