Bodi za elimu zapewa mtihani

12Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bodi za elimu zapewa mtihani

BODI za elimu za shule za msingi wilayani Handeni mkoani Tanga zimepewa miezi sita kuhakikisha kiwango cha elimu kinakua ili kuepuka bodi hizo kuvunjwa.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, wakati wa kikao cha wadau wa elimu wa halmashauri za wilaya za vijijini na mjini za wilaya hiyo kilichoandaliwa na ofisi yake kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wilayani humo.

Gondwe alisema bodi hizo ziandaliwe barua kukumbuka majukumu yao ili kupandisha kiwango cha ufaulu na bodi itakayoshindwa kufanya hivyo ndani ya muda uliopangwa, itavunjwa.

“Bodi za shule wilaya ya Handeni zisimamie ukuaji wa elimu kuanzia mwezi huu hadi Juni na itakayoshindwa itavunjwa kupitia ofisi za wakurugenzi,” alisema.

Aidha alisema kiwango cha ufaulu kwa mwaka 2017 walichojiwekea wilayani humo kilipanda na kuvuka lengo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 12, na katika kikao hicho wameazimia kiwango cha ufaulu kifikie asilimia 30 kwa mwaka huu.

Hata hivyo, baadhi wa walimu wakuu wa shule walieleza changamoto zinazowakumba katika shule zao na  kusema ongezeko la wanafunzi kwa mwaka huu ni kubwa ikilinganishwa na mahitaji ya shule.

“Mimi katika shule yangu nimeandikisha wanafunzi 1,085 kuanzia awali hadi darasa la saba, vyumba vya madarasa hatuna na tupo walimu 11 tu, tuna uhaba mkubwa wa walimu tulitegemea tutapata mwaka huu, lakini nimeambiwa walimu walikuja 24 na tayari wameshapangiwa shule mimi sikupata kabisa,” alisema Saidi Kiduo, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Sua.

Akijibu hoja hizo mkuu wa wilaya alisema Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 400 ili kupata uwiano wa ikama kwa walimu wa shule za msingi nchini, hivyo tatizo la uhaba wa walimu linashughulikiwa na litakwisha.

 

 

 

Habari Kubwa