Bil. 1/- kutengeneza barabara Mkuranga

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bil. 1/- kutengeneza barabara Mkuranga

WILAYA ya Mkuranga mkoani Pwani, imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kutengeneza barabara.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ullega.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ullega, katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani hapo.

Ullega ambaye ni mbunge wa Mkuranga, alisema kwamba ujenzi wa barabara utaanza mwezi huu kuanzia Mkuranga mjini hadi Kurungu.

“Mkuranga vijiji karibu vyote nilivyopita nimekuta changamoto ni barabara kuwa mbovu hata hivyo, tutaanza mwezi huu kwa kujenga barabara ya Mkuranga Mjini hadi Kurungu kwa kiasi cha Shilingi bilioni moja,” alisema.

Alisema barabara hiyo imekuwa ikiwapa wakati mgumu wananchi kufika hospitali kutokana na ubovu wake na kusababisha hata wamiliki wa vyombo vya moto kuwatoza nauli zisizoeleweka kutokana na ubovu wa barabara.

Alisema pia barabara hiyo iendayo hospitali imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kutokana na ubovu wake na vumbi kusababisha watu kutembea na kuchafuka kwa vumbi.

Pia Ullega alisema kuwa barabara za kuunganisha vijijini wanaziombea fedha ambapo mwaka huu zitaanza kutengenezwa. 

Habari Kubwa