Askofu Mkuu Methodisti afariki dunia

02Jan 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Askofu Mkuu Methodisti afariki dunia

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Methodisti nchini, Dk. Mathew Byamungu, amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia juzi katika hospitali ya Taifa ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Methodisti nchini, Dk. Mathew Byamungu.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kanisa la Methodisti, Askofu,Yusuf Bundala, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Dodoma, imeeleza alipelekwa Muhimbili akitokea TMJ baada ya kujisikia vibaya kutokana na maradhi ya kisukari yaliyokuwa yakisumbulia kwa muda mrefu na kufariki kabla ya kuanza kupatiwa matibabu.

Askofu Bundala alisema mipango ya mazishi inaendelea katika Kanisa Kuu la Methodisti la Msasani na anatarajiwa kuzikwa Januari 4, 2018 katika eneo la Kanisa la Methodisti la Boko.

Marehemu Byamungu alizaliwa1954 mkoani Kagera na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Kazilanfuka, Sekondari ya Kahororo na Mkwawa, kisha mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Chang’ombe jijini Dar es Salaam na baada ya kuhitimu alifundisha katika sekondari ya Azania jijini Dar es Salaam.

Alisema kati ya mwaka 1981-1984 alijiunga na Chuo Kikuu cha Asia Centre for Theological na kupata Shahada ya kwanza ya Theolojia na baada ya kuhitimu alirudi nchini na kufanya kazi ya uinjilishaji katika shule za sekondari na vyuoni jijini Dar es Salaam.Mwaka 1987-1989 alikuwa Mchungaji wa kanisa la KKKT. 

Mwaka 1990-1991 alisoma Shahada ya pili ya Theolojia katika Chuo Kikuu cha Hyup Sung, na pia mwaka 2009 alitunikiwa Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Latin California, Marekani.

”Mwaka 1991 alisimikwa kuwa Mchungaji wa kanisa la Immanuel Methodist la Korea na alipangiwa kuja kufanya kazi ya uinjilishaji Tanzania, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa kulisajili tawi la kanisa hilo nchini na kulibadilisha jina kutoka jina la awali la Tanzania Christian Methodist Church (TCMC) kuwa Tanzania Methodist Church (TMC) na kuongeza idadi ya waumini na makanisa ya Methodisti katika kipindi kifupi,” alisema.

Awaka 2003 alisimikwa kuwa Askofu wa kwanza wa kanisa hilo nchini nafasi aliyoendelea kuitumikia hadi mwaka 2009 alipoteuliwa kuwa Askofu Mkuu nafasi aliyokuwa nayo hadi kifo chake.

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa