Askofu Mkuu Lebulu astaafu, Massawe wa Moshi akimrithi 

28Dec 2017
John Ngunge
Nipashe
Askofu Mkuu Lebulu astaafu, Massawe wa Moshi akimrithi 

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu (75), aliyenusurika kufa kwa bomu lililolipuliwa kanisani, amestaafu rasmi. 

Askofu Josephat Lebulu

Lebulu alistaafu rasmi wadhifa wake kuanzia jana kwa mujibu wa utaratibu wa kanisa hilo wa askofi kustaafu katika umri huo, akiwa amelitumika Kanisa Katoliki kwa miaka 49 kama padre na miaka 38 kama askofu.

Askofu Mkuu Lebulu na mwenyeji wake wakati huo aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisko Padilla, walinusurika kufa Mei 5, 2013, baada ya mtu mmoja kuwarushia kitu kinachodaiwa kuwa bomu wakiwa wameanza ibada ya uzinduzi wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Katika tukio hilo, watu watatu walifariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa, wengine wakiachwa na ulemavu wa miguu na mikono.

Hadi kustaafu kwake jana, kwa mujibu wa sheria za kanisa hilo, Lebulu alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha tangu Machi 16, 1999.

Kabla ya hapo, alikuwa Askofu wa Jimbo la Arusha kuanzia mwaka 1998 kabla ya kupandishwa hadhi na kuwa jimbo kuu. Pia alikuwa Askofu wa Jimbo la Same tangu mwaka aliposimikwa Mei 24, 1979 kutokana na kuteuliwa na Papa Februari 12, 1979. 

Askofu Mkuu Lebulu ambaye alizaliwa Juni 13, 1942 alipata daraja la upadri Desemba 11, 1968 huko Same mkoani Kilimanjaro. 

Kutokana na kustaafu huko, tovuti ya Radio Vatican, ilisema jana kuwa Baba Mtakatifu Francisko, amemteua Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Isaac Amani Massawe, kuwa Askofu Mkuu mpya wa Jimbo Kuu la Arusha.

Padre Richard Mjigwa, C.PP.S wa Dar es Salaam, anayeshughulikia Habari za Vatican, alithibitisha kustaafu kwa Lebulu na uteuzi wa Askofu Mkuu mpya Massawe.

Askofu mkuu mteule Massawe, alizaliwa tarehe Juni 10, 1951 huko Mango, Jimbo Katoliki la Moshi.

Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, alipadrishwa Juni 29, 1975 na Novemba 21, 2007 aliteuliwa na Baba Mtakatifu (mstaafu Benedict XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi na kuwekwa wakfu Februari 22, 2008 na Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam akisaidiana na Askofu Mkuu Lebulu, pamoja na Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi (sasa marehemu).

Askofu Mkuu mteule, alisoma Shule ya Msingi Mango, Kibosho; Seminari Ndogo ya St. James, Moshi; Falsafa kati ya mwaka 1970 – 1972 katika  Seminari Kuu ya Ntungamo, Seminari Kuu ya  Kipalapala kati ya mwaka 1972 – 1975 na hatimaye kupadrishwa Juni 1975.

Akiwa Padri aliwahi kuwa Paroko wa Usu, mwalimu na mlezi wa Seminari Ndogo ya St. James, Moshi na kati ya mwaka 1986 hadi 1989 alikuwa masomoni Chuo Kikuu cha Walsh, Marekani.

Kati ya mwaka 1990 hadi 2003, alikuwa mlezi wa watawa na baadaye akateuliwa kuwa Paroko wa Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi.

Habari Kubwa