Anaswa akiuza vipodozi vya sumu 

24Dec 2017
Rose Jacob
Nipashe Jumapili
Anaswa akiuza vipodozi vya sumu 

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) Ofisi ya Kanda ya Ziwa imetishia kumnyang’anya leseni ya kufanya biashara ya vipodozi (jina tunalo)  , baada ya kumkuta anauza vipodozi vyenye viambata vya sumu.

Meneja wa TFDA Ofisi ya Kanda ya Ziwa,  Moses Mbambe,alisema kuwa mfanyabiashara huyo mmiliki wa duka la kuuza vipodozi lililoko Mtaa wa Lumumba jijini Mwanza amekuwa akikiuka sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 ya mwaka 2003 mara kwa mara.

Mbambe alisema kuwa katika ukaguzi uliofanyika hivi karibuni katika duka hilo walikamata vipodozi vyenye viambata vya sumu tani tatu vyenye thamani ya Sh. milioni 16.8.

 “Tulipokea taarifa kutoka kwa wananchi wenye mapenzi mema kuwa kuna duka mtaa wa Lumumba linauza vipodozi vilivyopigwa marufuku. Tulipofanya ufuatiliaji tulibaini kuwa ni kweli kuna bidhaa hizo dukani na na  stoo. Na hii haikuwa mara ya kwanza kwa duka hilo kukutwa na bidhaa ambazo haziruhusiwi” alisema Mbambe.

Alisema kuwa halikuwa tukio la kwanza kumkagua mfanyabiashara huyo na kumkuta na bidhaa hizo haramu. “ Katika ukaguzi tuliofanya katika duka lake   Novemba 2015 kufuatia taarifa za wasamalia wema tulikuta vipodozi vyenye viambata vya sumu vyenye thamani ya Sh milioni 27.3.

“Tulifunga duka hilo kwa muda na kumtaka alipe gharama za kuteketeza bidhaa hizo ambapo alilipa asilimia 25  ya thamani ya bidhaa alizokutwa nazo kama kifungu cha 99 (1) cha sheria ya chakula, dawa na vipodozi kinavyoelekeza. Inaonekana adhabu hii haikumsaidia kubadilika. Tutaanza mchakato wa kumnyang’anya kibali kama tutamkuta tena anauza bidhaa zilizopigwa marufuku” alisema.

Mbambe aliongeza kuwa tayari wamemuandikia barua ya onyo la mwisho mfanyabiashara huyo na kuwa kama atarudia tena kosa hilo watamchukulia hatua zaidi ikiwamo kumnyang’anya leseni yake ya kufanya biashara ya vipodozi.

Habari Kubwa