Aliyeshinda CCM kumrithi  Nyalandu akwama kortini 

14Dec 2017
Elisante John
Nipashe
Aliyeshinda CCM kumrithi  Nyalandu akwama kortini 

HAIDER Gulamali, mwanaCCM aliyekuwa akiwania kumrithi aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, alifikishwa kortini jana baada ya kukamatwa juzi mjini hapa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akituhumiwa kutoa rushwa ya Sh. milioni mbili. 

Aliyekuwa mtia nia ya ubunge wa jimbo la Singida Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi, Haider Gulamali (katikati) akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa Takukuru Mkoa wa Singida baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kumhonga ofisa usalama wa taifa Sh. milioni mbili, ili asaidie kuthibitishwa kwa jina lake na vikao vya juu vya CCM.

Akizungumza na Nipashe kwa simu akiwa Dodoma jana jioni, Ofisa Uhusiano wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba,  alisema Gulamali alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida jana mchana mbele ya Hakimu Flora Ndale na kusomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Edson Mapalala.

Mshtakiwa ambaye kwa mujibu wa Misalaba ni mfanyabiashara wa viwanda vya magodoro mjini Dodoma, alikana mahakamani shtaka la kutoa rushwa juzi saa 8:30 mchana.

Misalaba alisema: "Mshtakiwa alikamatwa juzi kwa kutoa rushwa ya Sh. milioni mbili kwa Kiseo Nzowa, ili amsaidie kushinda uchaguzi Singida Kaskazini na alishapita kwenye kura za maoni."

Kwa mujibu wa Misalaba, mshtakiwa anatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Godfrey Wasonga.

HATIMA YA DHAMANAOfisa huyo wa Takukuru aliongeza kuwa upande wa mashtaka ulipinga mshtakiwa kupewa dhamana kwa maelezo kuwa atavuruga mchakato wa uchaguzi licha ya kwamba chama chake tayari kimeshatengua ushindi wake alioupata katika kura za maoni.

Misalaba alisema kesi hiyo iliahirishwa hadi leo Mahakama itakapotoa uamuzi kama mshtakiwa anastahili dhamana au la.

ALIVYOKAMATWA 

Awali jana asubuhi Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joshua Msuya, aliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa jinsi walivyomnasa mfanyabiashara huyo.Alidai walimkamata mjini hapa kwa tuhuma za  kutoa rushwa ya Sh. milioni mbili baada ya kumwekea mtego.

Gulamali, mkazi wa Dodoma, alishinda kwenye kura za maoni zilizopigwa Jumapili akiwania kiti hicho kilichobaki wazi baada ya Nyalandu kujiuzulu na kuomba kuhamia upinzani Oktoba.

Ilielezwa na 'kigogo' huyo wa Takukuru kuwa mwanaCCM huyo kabla ya kufikishwa kortini jana mchana, alikuwa anashikiliwa kwa tuhuma ya kumpatia rushwa ofisa usalama wa taifa mmoja ili amsaidie kuthibitishwa na vikao vya juu.

Msuya aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa Gulamali alikamatwa juzi saa nane alasiri kwenye hoteli moja mjini hapa akiwa na ofisa huyo.

“Tunamshikilia Haider Hussein Gulamali, alishawishi kumpa rushwa ofisa usalama wa taifa," alisema Msuya na kwamba "aliendelea kuwasiliana naye, lakini kutokana na mtego tuliouandaa, tulimkamata baada ya kukabidhi fedha hizo Sh. milioni mbili.”

Alisema kukamatwa kwa mtia nia huyo kulitokana na kupata taarifa iliyotaka ofisa huyo akamtolee habari nzuri kwenye ngazi za juu ili athibitishwe na vikao husika kugombea Jimbo la Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM.

Mkuu huyo wa Takukuru alisema uchunguzi zaidi unaendelea na utakapokamilika, Gulamali atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kujibu tuhuma zinazomkabili.Aidha, Msuya alisema uchunguzi zaidi unaendelea kufuatilia tuhuma za vitendo vya rushwa dhidi ya mtuhumiwa anavyodaiwa kufanya kabla na baada ya upigaji kura za maoni Jumapili.Nyalandu, waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, alitangaza kuachia ubunge wa Sindiga Kaskazini na kuihama CCM Oktoba 30 kisha kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kile alichodai kutoridhishwa na mwenendo wa sasa wa chama hicho tawala.

Lakini siku mbili baadaye, taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, ilieleza kuwa hakupokea barua ya Nyalandu kujiuzulu nafasi yake.

Aidha, Ndugai alisema alichopokea ni barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ya Oktoba 30 ikimwarifu kuwa Nyalandu amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa ibara ya 13 ya katiba yao.

Kutokana na taarifa ya Kinana, Ndugai aliiarifu Tume ya Uchaguzi (NEC) kuwa jimbo la Singida Kaskazini lipo wazi.

Ndipo NEC ilipotangaza ratiba ya uchaguzi mdogo katika majimbo, pamoja na Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini na kata sita za Tanzania Bara ambao utafanyika Januari 13, mwakani.

Akitoa taarifa kwa umma jijini Dar es Salaam Desemba 2, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid, alisema tume imetangaza uchaguzi huo baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika ya kwamba nafasi hizo ziko wazi.

Jaji Hamid alitaja ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo kuwa utoaji fomu ni Desemba 12 hadi 18 isipokuwa kwa jimbo la Songea Mjini ambako utoaji fumo ni kuanzia leo hadi Jumatano ijayo.

Kampeni za uchaguzi huo katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na kata zote sita zitaanza Jumanne na kumalizika Januari 12, alisema. 

Katika jimbo la Songea Mjini, hata hivyo, kampeni zitaanza Alhamisi ijayo na kumalizika pia Januari 12, alisema jaji mstaafu huyo.

TENGUA MATOKEO

Kinyang'anyiro cha kumtafuta mrithi wa Nyalandu ndani ya CCM kwa ajili ya uchaguzi huo kilianza Jumapili kwa kura za maoni ambazo Gulamali alishinda, lakini mbali na kukamatwa na Takukuru, chama hicho kimetengua matokeo hayo na kuagiza uchaguzi mwingine.  

Mshindi wa kura za maoni ndani ya CCM anatarajiwa kuingia bungeni bila jasho baada ya upinzani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusema hautashiriki uchaguzi huo kama NEC haitakaa nao kujadili kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa marudio wa madiwani mwezi uliopita.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika kata 43 za Tanzania Bara, CCM ilishinda viti vyote isipokuwa kimoja cha wilayani Rungwe.

Katika kura za maoni zilizopigwa katika tarafa ya Ilongero, Gulamali aliibuka mshindi kwa kuzoa kura 606 kati ya 1,010 za wajumbe, akiwaacha mbali wagombea wengine 21 akiwamo Justine Monko aliyemfuatia kwa kura (133) na Juma Mgoo (46).

Kura mpya za maoni sasa zitapigwa na halmashauri kuu ya Jimbo badala ya mkutano mkuu wa Jimbo ili kuwahi mchakato wa Nec, taarifa ya CCM juzi ilisema.

 

Habari Kubwa