800 wapimwa, kutibiwa bure

29Nov 2016
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
800 wapimwa, kutibiwa bure

WANANCHI 800 wa Kerege Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, wamejitokeza kupima magonjwa mbalimbali yakiwamo yasiyoambikiza kama shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya njia ya mkojo na kupatiwa matibabu bure.

Kati ya wagonjwa hao, saba walikutwa na matatizo kwenye njia ya mkojo na kusafirishwa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa matibabu zaidi.

Huduma ya matibabu pamoja na zawadi mbalimbali ilitolewa na Klabu ya Rotary ya Oysterbay kwa kushirikiana na madaktari na wafanyakazi wa kujitolea.

Rais wa Klabu ya Rotary ya Oyster Bay, Alfred Woiso, akizungumza juzi wakati wa utoaji huduma hiyo, alisema vipimo na matibabu vilitolewa bure kwa magonjwa kama vile malaria, upungufu wa damu, kisukari na shinikizo la damu, masikio, pua, koo, magonjwa ya ngozi, macho pamoja na meno.

Alisema huduma nyingine zilizotolewa zilikuwa pamoja na ugawaji wa miwani zilizotolewa kwa watu waliokutwa na matatizo ya macho.

Woiso alitaja huduma nyingine kuwa ni za ushauri kwa wajawazito na vifaa vya kujifungulia vilivyotolewa bure kwa wajawazito, huduma za ushauri nasaha, upimaji wa Virusi vya Ukimwi na elimu ya usafi na taulo za wanawake zilitolewa kwa wasichana.

“Ni furaha yetu kuwa hapa kwa mara nyingine tena na tunafurahi kuona wakazi wa Kerege wamejitokeza kuja kupata huduma hizi.

Tumetoa huduma kwa watu waliokuwa na matatizo mbalimbali. Tumeona wagonjwa wengi wenye magonjwa sugu kama kisukari na shinikizo la damu na inaonekana kuna haja ya kupanua wigo wa huduma zetu kwa vile kuna mahitaji ya huduma za matibabu ya magonjwa mengine,” alisema Woiso.

Mtaalamu wa Dawa na Tiba, Dk. Sajjad Fazel, kutoka Hospitali ya Sanitas, alisema wagonjwa wa rika zote walijitokeza kupata huduma za matibabu na kwamba huduma ya upimaji wa malaria ilitolewa kwa kila mwananchi aliyejitokeza.

Alisema madaktari 90 wakiwamo bingwa kutoka hospitali mbalimbali za serikali na zile za binafsi 30 na wanafunzi wa udaktari 60 walishiriki kutoa huduma hiyo.

Kambi hii inayoandaliwa na Klabu ya Rotary ya Oysterbay imefanyika Kerege kwa mara ya sita, kwa lengo la kuwasaidia wakazi hao kupata huduma za matibabu, kutokana na wengi wao kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Kambi hiyo ya matibabu imedhaminiwa na Diamond Trust Bank (DTB) na kuandaliwa kwa ushirikiano na Shree Hindu Mandal Hospital, Vital Supplies, Whitedent, vClick Concepts Inc, MAK Books and Brains, Abacus Pharmaceuticals, Fazel Foundation na wanachama wa Klabu ya Rotary.

Habari Kubwa