13,600 wakutwa na homa ya ini

23May 2019
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
13,600 wakutwa na homa ya ini

KATI ya wachangiaji wa damu 307,835, waliojitokeza kuchangia damu katika vituo mbalimbali nchini mwaka jana, watu 13,613 (asilimia 4.4) walibainika kuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya ini aina ya Hepatitis B na 1,092 virusi aina ya Hepatiti C.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Catherine Sungura, virusi vya kundi B na C vinapoingia kwenye mwili wa binadamu kushambulia ini na baadhi hawaonyeshi, hupata athari kwenye ini na wengine kupata maambukizi sugu na wa muda mrefu.

 

Aidha, takwimu hizo zilieleza kuwa, katika kipindi cha mwaka juzi kati ya watu 233,953 waliojitokeza kuchangia damu, watu 11,417 (asilimia 4.9) walikuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya ini aina B.

“Katika jamii, utafiti mahususi ujulikanao kama ‘This Tanzania HIV Indicator Survey’ uliratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, mwaka 2016/17 ulionyesha maambukizi ya homa ya ina aina ya B ni asilimia 4 miongoni mwa Watanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49,” alieleza Sungura katika taarifa hiyo.

Alisema virusi hivyo vya kundi B, C na D huambukizwa kwa njia ya kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana na wenye maambukizi na kujidunga sindano yenye virusi vya ugonjwa huo.

Alitaja njia nyingine za maambukizi ni majimaji yenye uambukizo kama damu na matapishi kutoka kwa mgonjwa mwenye virusi hivyo na kuingia kwa mtu mwingine andapo ana kidonda au michubuko ya ngozi.

Alisema njia zinazoeneza virusi vya homa ya ini ni zile zinazoeneza Ukimwi ikiwamo mama anapoweza kumuambikiza mtoto wakati wa ujauzito na kujifungia.

“Taarifa hii pia inabainisha na kufafanua ukweli juu ya ugonjwa huu kufutia taarifa potofu zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ugonjwa huu na namna ya kujikinga,” alisema Sungura.

Kuhusu dalili za ugonjwa huo, alisema mtu anaweza kuugua na asiwe na dalili na hufanya hivyo pindi unapokolea mwilini ambazo ni mwili kuishiwa nguvu, kichefuchefu na kutapika, homa ya tumbo.

Alisema hatua zinazochukuliwa na serikali ni kutoa chanjo kwa watoto wadogo, kwa watu walio katika hatari ya kupata maambukizi na kwamba wameanza kutoa chanjo hizo kwenye vituo vya afya nchini.

Habari Kubwa