Watoboa siri ushindi Chadema

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
    Watoboa siri ushindi Chadema

VIONGOZI wa mila wa jamii ya Kimasai maarufu kwa jina la Laigwanani, wilayani Longido, wametoboa siri ya ushindi wa Chadema katika uchaguzi mkuu uliopita wakidai asilimia kubwa ya ushindi huo ulipatikana kwa wizi kwa kutumia mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chadema ilishinda katika uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Longido kupitia mgombea wake Onesmo ole Nangole, lakini Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, ilitengua ubunge huo baada ya kugundua kasoro mbalimbali za uchaguzi ikiwamo wizi wa kura.

Mmoja wa Laigwanani aliyejitambulisha katika mkutano wa hadhara wa CCM wa kuomba kura uliofanyika katika Kata ya Orbomba, Tapilit ole Mokoro, alidai Chadema waligundua aliyekuwa mgombea wa CCM Dk. Stephen Kiruswa, ana nguvu hivyo walifanya kila namna ya hila ili waibuke washindi.

Alisema na kuitahadharisha CCM kuwa makini na mawakala wao kwa kuwa sifa kubwa ya ushindi katika chaguzi ni kuweka mawakala wenye sifa za kulinda kura za mgombea wake na wasiokuwa na tamaa ya kurubuniwa na wapinzani.

Hata hivyo, aliowamba wakazi wa jimbo hilo kumsamehe kwa sababu alienda upinzani kwa kufuata mkumbo na hakufanya hivyo kwa sababu anaichukia CCM.

“Nisameheni na chukueni hiyo kama changamoto ya maisha kwa kuwa wengi mwaka 2015, tulihama CCM kwa kumfuata mtu mmoja bila kujijua kuwa huo ni umbumbu,’’ alisema.

 

Habari Kubwa