Wilaya yakosa mafuta siku 4

17Jul 2017
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Wilaya yakosa mafuta siku 4

JANA ilifika siku ya nne bila upatikanaji wa mafuta katika wilaya ya Muheza baada ya vituo vyake vyote vinne kufungwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kutokana na mashine zake kutokuwa na mashine maalumu za kielektroniki za kutolea risiti.

Wakati hali wilayani Muheza ikiwa mbaya, watumiaji wa magari na pikipiki wa mkoa wa Dodoma jana walipata ahueni ya ukosefu wa nishati ya petroli na dizeli baada ya vituo vyake kuruhusiwa kuendelea na biashara kwa udhaini wa Mkuu wa Mkoa.

Wilaya ya Muheza ina vituo vya kuuza mafuta vinne tu ambavyo vyote vimefungwa na TRA mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na TRA wilaya ya Muheza, baada ya kuvikagua mwishoni mwa wiki iliyopita na kukuta havina mashine hizo za risiti za kisasa.

Tukio hilo la kufunga vituo hivyo vyote vinne wilaya ya Muheza lilifanyika juzi majira ya saa 10:00 jioni baada ya maofisa wa TRA mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na wilaya ya Muheza kufanya ukaguzi katika vituo hivyo vya mafuta.

Vituo hivyo vya mafuta vilivyofungwa ni kituo cha kuuzia mafuta cha COPEC, kituo cha kuuza mafuta cha Mvuleni, kituo cha kuuzia mafuta cha Puma na kituo cha kuuzia mafuta cha Kwamnyamuru kilichopo Muheza ndani.

Kutokana na kufungwa kwa vituo hivyo vya kuuzia mafuta wilayani Muheza, wamiliki wa vyombo vya usafiri ikiwamo magari na pikipiki wamelazimika kwenda katika vituo vya wilaya za Tanga na Korogwe kupata huduma hiyo na madereva wengine wa bodaboda kuzifungia ndani.

Ramadhani Juma, mkazi wa Majengo wilayani Muheza ambae anafanya kazi ya kuendesha bodaboda alisema wanalazimika kwenda kununua mafuta Tanga mjini ambako ni umbali wa kilomita 40 kutoka Muheza.

Alisema kuwa kuna walanguzi wanaokwenda kununua mafuta hayo jijini Tanga kwa wingi na kuyaleta wilayani Muheza ambapo wamekuwa wakiuza lita moja kwa Sh. 3,000 badala ya Sh. 2,100 ambayo ni bei kikomo elekezi.

Kwa upande wake, John William, mkazi wa Mdote alisema kuwa anamiliki gari ndogo, lakini kutokana na kukosa mafuta vituoni amelazimika kuliegesha gari hilo.

Meneja wa TRA wilaya ya Muheza, Swalehe Byarugaba alisema zoezi la kufunga vituo vya mafuta ambavyo havina mashine za kielektroniki ni agizo la serikali na kwamba ni endelevu katika mkoa wa Tanga.

Aliwataka wafanyabiashara wa mafuta na wengine kununua mashine hizo za kisasa za kutoa risiti ili kuhakikisha serikali inapata mapato ya kusaidia kuendeleza nchi.

Mjini Dodoma, wafanyabiashara wa mafuta wameagizwa kuhakikisha wanafunga mashine hizo kwenye vituo vyao ndani ya siku 10 na endapo watashindwa vitafungwa.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana wakati wa kikao chake na Meneja wa TRA mkoani humo, Thomas Masese na viongozi wa chama cha wafanyabiashara wa mafuta wa mjini hapa.

Rugimbana alisema kufungwa kwa mashine hizo kutaiwezesha serikali kukusanya kodi kikamilifu.

Aliwataka wamiliki wote wa vituo kuhakikisha ndani ya siku hizo wanafunga mashine hizo na kuahidi kushirikiana na TRA kuweka msukumo mashine hizo zipatikane kwa haraka na kufungwa kwenye vituo vya mafuta.

“Wapo ambao wamekwisha nunua mashine hizo na sasa wanasubiri kufungiwa kwenye vituo vyao, na pia wapo wale waliolipia mashine hizo kwa mawakala wa TRA na wanasubiri kuletewa mashine hizo,” alisema Rugimbana akielezea sababu ya kulegezwa kwa agizo la Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango la katikati ya wiki iliyopita.

MWAMKO MZURI
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Dodoma, Thomas Masese alisema vituo vingi vimeshafunga mashine hizo na vichache vinasubiri kuletewa ili vifunge.

Alisema wafanyabiashara wa mkoa huo wana mwamko mzuri wa ulipaji kodi kwa kutumia mashine hizo.

Masese alisema mwamko huo ndiyo uliochangia Mamlaka hiyo mkoani humo kuvuka lengo katika ukusanyaji kodi kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni.

Alisema mkoa ulipangiwa kukusanya Sh. bilioni 47, lakini makusanyo yalivuka na kufikia Sh. bilioni 52.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Kanda ya Kati, Faustine Mwakalinga aliishukuru serikali ya mkoa kwa kutoa muda huo ili kukamilisha ufungaji wa mashine hizo.

Dk. Mpango aliiagiza TRA kufanya ukaguzi nchi nzima ili kubaini wamiliki wa vituo vya mafuta wanaokiuka maagizo ya Serikali yaliyowataka wafunge EFD tangu mwaka jana, Jumatano iliyopita.

Dk. Mpango alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Manispaa ya Ilala, Jijini Dar es Salaam.

Katika eneo hilo, Dk. Mpango aliamuru kituo cha mafuta cha GBP kifungwe hadi hapo kitakapofunga mashine za EFD.
Alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kituo hicho hakikuwa kikitumia ipasavyo mashine za EFD.

Kituo hicho chenye pampu nne za mafuta kilikutwa na mashine moja ya mkononi ya EFD.

Jambo hilo, alisema Dk. Mpango, husababisha wateja wengi kutopewa risiti na hivyo kuikosesha Serikali mapato yake na ni "kinyume cha sheria za nchi".

“Sasa nawachukulia hatua ili liwe fundisho kwa wengine wote wanaouza mafuta nchini bila kufuata taratibu," alisema Dk. Mpango.
"Na nitaanza na wewe.

"Biashara yako isimame mpaka mashine zifungwe kwenye kituo chote na utekeleze mara moja.”

Mapema mwaka jana, TRA ilitoa agizo kwa vituo vyote vya mafuta nchini viwe vimefunga mashine za EFD ambazo zimeunganishwa moja kwa moja kwenye pampu kufikia Machi mosi, 2016.

Kufuatia tangazo hilo, uongozi wa Chama cha Wamiliki na Waendeshaji wa Vituo vya Mafuta (TAPSOA) ulikutana na TRA na kuibuka na makubaliano ya pamoja ambayo yaliacha mwanya wa baadhi ya vituo kutoanza kutumia EFD za kwenye pampu "wakati changamoto za kiufundi, mtandao na bei za EFD zikishughulikiwa".

* Imeandikwa na Steven William, MUHEZA na Augusta Njoji, DODOMA

Habari Kubwa