Waziri atangazia vita wauza mbegu feki  

31Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Waziri atangazia vita wauza mbegu feki  

NAIBU Waziri wa Kilimo, Mary Mwanjelwa, ametangaza vita dhidi ya  wafanyabiashara wanaouza mbegu feki zilizopigwa marufuku na serikali kwa kuwa ni chanzo cha kuzorota kwa sekta hiyo. 

Akizungumza juzi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Morogoro, Mwanjelwa aliwataka wafanyabiashara wote wa mbegu ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa njia zisizo halali, kuacha mara moja. 

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiwauzia wakulima mbegu  zilizopigwa marufuku. Aliwataka kuacha haraka iwezekanavyo kwa kuwa wakibainika serikali itawachukulia hatua za kisheria.

"Serikali imepokea malalamiko mengi kwa wananchi kuhusu ubovu wa mbegu, jambo ambalo limesababisha kwa kiasi kikubwa kuwa na mavuno kidogo pasina kukidhi matakwa ya wakulima wetu nchini," alisema.

Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, alitembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), ambayo imepewa jukumu na serikali kusajili   wafanyabiashara wa mbegu.

Katika taasisi hiyo, Naibu Waziri aliiagiza TOSCI kujitathmini kwa utendaji duni kwa kuwa imeshindwa kutimiza majukumu yake kwa kuwabaini wafanyabiashara wanaokiuka maagizo ya serikali pamoja na taratibu na sheria za nchi.

Aidha, aliitaka taasisi hiyo kuwafuatilia upya wafanyabiashara wote wa mbegu nchini ili kubaini wanaokiuka matakwa ya serikali na kutaka kukwamisha juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli. 

Pia aliwataka watumishi kutofanya kazi kwa mazoea badala yake kuongeza uadilifu, uaminifu, juhudi, ubunifu, nidhamu na uzalendo katika utendaji kazi.

 

 

Habari Kubwa