Wanging’ombe wafaidika mil. 400/- huduma za afya

03Jan 2018
Furaha Eliab
Nipashe
Wanging’ombe wafaidika mil. 400/- huduma za afya

HALMASHAURI ya Wilaya ya Wanging’ombe imepatiwa Sh. milioni 400 na Benki ya Dunia kwa ajili ya ukarabati wa huduma za afya katika Hospitali ya Palangawano inayohudumia wakazi wengi kwa wakati mmoja.

Hospitali hiyo inatumika kama ya wilaya kutokana na halmashauri hiyo kukosa hospitali ya wilaya.

Kutokana na msongamano katika hospitali hiyo, wagonjwa hulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya katika hospitali ya binafsi ya Ilembula inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT) ambako gharama za matibabu zikidaiwa kuwa ni juu, huku gharama za matibabu zikitajwa kuwa na kuwaathiri wagonjwa hususani wajawazito.

Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe, Gerson Lwenge, alisema kandarasi kwa ajili ya ukarabati wa hospitali hiyo imeshatangazwa kwa ajili ya kupanua huduma kwa wakazi wa halmashauri hiyo.

Lwenge anatoa kauli hiyo wakati akitoa tathmini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Wanging’ombe huku akisema hiyo ni moja ya hatua walizofikia.

Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa mama na mtoto wanakuwa salama kwa kupata huduma karibu na maeneo yao na kuondokana na kusafiri umbali mrefu hasa mama akiwa anataka kujifungua.

“Baada ya kukamilika kwa ukarabati Benki ya Dunia imeahidi kutupa vifa vya Sh. milioni 300 kwa ajili ya kutoa huduma bora zenye viwango,” alisema.

Hata hivyo, mkuu wa wilaya hiyo, Ally Kasinge, alisema wilaya yake ina mikakati ya kuboresha huduma za afya na halmashauri inatarajia kujenga zahanati kumi na vituo vya afya vinne.

 

 

 

Habari Kubwa