Wamiliki viwanda wapata neema

09Apr 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Wamiliki viwanda wapata neema

SERIKALI imetangaza neema kwa wamiliki wa viwanda na kampuni kwa kuahidi kushughulikia changamoto tisa zinazowakabili ikiwamo kuanza kuwashirikisha katika kufanya maamuzi juu ya mabadiliko ya sheria na sera ili kuwaepusha na uwezekano wa kupata hasara.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Dk. Reginald Mengi, akitoa neno la shukrani.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alitoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa wazalishaji bora wa viwanda.

Tuzo hizo ziliandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) huku mdhamini mkuu akiwa ni Benki M na baadhi zikiwa ni kampuni ya The Guardian kupitia magazeti yake ya The Guardian na Nipashe, Televisheni ya ITV pamoja na kampuni ya Coca Cola ambazo zilipewa vyeti vya udhamini.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa CTI, Shabbir Zavery, alitaja changamoto tisa zinazowakabili wamiliki wa viwanda nchini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Samia alisema serikali inatambua kwamba sekta binafsi inapaswa kushirikishwa kwenye mabadiliko ya sheria na sera kwa kuwa ni lazima waende pamoja ili kukuza uchumi wa nchi.

“Wafadhili tuliokuwa tunawategemea watukopeshe nao wana shida kwao ya kiuchumi, hivyo lazima tutafute vyanzo vya mapato na ndiyo maana serikali mwaka jana ilibadilisha sera… ila tutatoa maelekezo ili tuende pamoja kwa sababu ile ilikuwa mwaka wa kwanza wa awamu ya serikali hii,” alisema Samia.

Kuhusiana na changamoto ya kuwapo kwa utitiri wa kodi kutoka kwenye mamlaka za ukaguzi na udhibiti wa bidhaa za viwanda, kilimo, utalii na biashara nyingine, Samia alisema serikali inalifanyia kazi suala hilo.

“Niseme nimekutana na changamoto hii katika ziara zangu mikoani ambako nimepata fursa ya kutembelea miradi na viwanda kadhaa … niliwahi kusema mamlaka hizo zote ni za serikali hivyo wanaweza kukaa pamoja na kuona namna ya kuondoa adha hii,” alisema.

Pia alimtaka Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage kuhakikisha taarifa ya maboresho ya sheria zinazokinzana inakamilika haraka iwekezanavyo.

Kuhusu changamoto ya kutorejeshewa malipo stahiki wanayodai Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mama Samia alisema jambo hilo litafanyiwa kazi.

Pia alisema tatizo la uzalishaji mdogo wa makaa ya mawe limeshughulikiwa na hivyo uzalishaji utaongezeka wiki ijayo ili kukidhi mahitaji.

Aliwaahidi wamiliki wa viwanda kuwa atahakikisha anakuwa karibu na Waziri Mwijage ili kuhakikisha kuwa yote yaliyoahidiwa katika kukabiliana na changamoto zilizotajwa yanatekelezwa.

Aidha, Mama Samia aliwataka Watanzania kupenda kununua bidhaa za ndani ili kukuza viwanda.

Awali, Mwenyekiti wa pili wa Mwenyekiti wa CTI, Zavery, alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni mabadiliko ya mara kwa mara na ghafla ya sera au sheria za kibiashara ambazo huondoa utulivu kwa wazalishaji; kuwapo kwa wingi wa mamlaka za udhibiti; uchakavu na ukosefu wa miundombinu ya usafiri wa reli na kuchelewa kutoa mizigo bandarini; kutorejeshewa malipo stahiki wanayodai TRA na pia kodi zinazoua ushindani mfano ni utozwaji wa kodi ya ongezeko la thamani kwa malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa dawa, mbolea na vyandarua wakati dawa na mbolea zinazoingizwa nchini hazitozwi kodi.

Zavery alisema changamoto nyingine ni agizo la serikali la kupiga marufuku ununuzi wa makaa ya mawe kutoka nje ilhali yaliyopo nchini hayakidhi mahitaji; utoaji wa vibali vya kufanya kazi na vya makazi na nyingine ni ubomoaji wa majengo yaliyopakana na reli ya kati hivi karibuni ambapo miongoni mwa waliobomolewa ni wanachama wa CTI ambao wanalalamika kuwa yalikuwa kwenye viwanja halali .

DK. MENGI AIAHIDI SERIKALI
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi, aliiahidi serikali kuwa sekta binafsi itakuwa bega kwa bega nayo ili kuhakikisha taifa linaifikia ndoto ya kuwa na uchumi wa viwanda. Alisema ni vyema kila Mtanzania akafikiria viwanda.

“Mwanzo ni mgumu, fikiria kitu kikubwa zaidi lakini ukaanza polepole na hatimaye ukafikia malengo ya kuwa na kiwanda kikubwa,” alisema Dk. Mengi.

“Makamu wa Rais Suluhu… miaka mingi wanaume tulifikiria wanawake hawawezi lakini wana uwezo mkubwa. Tuna imani tukiwa nawe na Rais John Magufuli tutashinda,” alisema.

Awali, Waziri Mwijage alisema wizara yake tayari imeunda kamati kuhusu changamoto ya kuwapo kwa utitiri wa mamlaka za ukaguzi na uthibiti ili ifanyiwe kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga, alisema wenye viwanda wana dhamira ya dhati ya kujenga Tanzania ya viwanda na hivyo akaitaka serikali kuchukua hatua madhubuti ya kuondoa vikwazo vilivyopo.

WASHINDI WA TUZO
Mbali na TBL waliotwaa tuzo ya jumla na ile ya makampuni makubwa, washindi wengine katika tuzo za jumla ni Mufindi Paper Mills iliyoshika nafasi ya pili na Kioo Limited iliyotwaa nafasi ya tatu.

Baadhi ya kampuni zilizoshiriki kwenye maonyesho ya kabla ya hafla hiyo ni Amorette ya Jacqueline Mengi, ambaye ni mke wa Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi.

Habari Kubwa