Waliohodhi maeneo uchimbaji kufutiwa leseni

19Jun 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waliohodhi maeneo uchimbaji kufutiwa leseni

SERIKALI imesema itawafutia leseni wawekezaji wakubwa  na wakati  waliohodhi  maeneo  ya uchimbaji wa madini  bila kuyafanyia
kazi kwa muda mrefu.

Kauli  hiyo ilitolewa  na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa, Yahaya  Samamba,  wakati  wa mafunzo  ya kuwajengea weledi  katika  utendaji  wachimbaji wadogo mkoani Geita.

Alisema serikali  haitasita  kuwafutia leseni  wawekezaji  hao na maeneo  yao kupewa wachimbaji wadogo iwapo  hawatajitokeza na kuanza kuyaendeleza.
Samamba  alisema baadhi  yao wamepewa leseni za umiliki na utafiti kisha kuyatelekeza wakati wachimbaji  wadogo hawana  maeneo  ya kufanya kazi.

Pia amewaonya  wamiliki  wa migodi watakao sababisha ajali za kizembe katika maeneo  ya kazi  kuwa serikali itawachukulia hatua za kisheria pamoja na kuwafutia leseni zao itakapo bainika kuwa chanzo ni uzembe wao.

Pia aliwataka  wachimbaji wadogo  na wakati  kulipa kodi  kwa hiari bila kusukumwa ili serikali ipate  mapato  huku akisisitiza wachimbaji  kudhibiti uchafuzi wa mazingira na  uchimbaji holela.

“Nasema wajitokeze  wenyewe mapema  kama wanataka kuyaendeleza  na kama   hawawezi  kuyafanyia kazi maeneo hayo warudishe serikali iwape wachimbaji wadogo,” alisema  Samamba.

Mkaguzi  wa migodi, Ally  Maganga, alisema takwimu  za ajali katika migodi  ya mkoani Geita  zinaonyesha mwaka 2008 ajali zilikuwa   mbili hadi nne  na 2014/2015  ajali 15   Juni  2016 hadi  Juni 2017  kuna idadi 16 hadi 20 ambapo watu zaidi  ya 18 walipoteza maisha.

Alisema kuwa  ajali  ya  miamba  kuporomoka  na kifusi ni asilimia 58% na kukosa hewa ina changia kwa asilimia 21% na kwamba  ajali zingine
zinasababishwa  hitirafu  ya umeme na uchimbaji holela kwa wachimbaji wadogo, hivyo  aliwataka  wamiliki wa migodi kuajiri  watalaamu wa umeme kudhibiti  hali hiyo .

Mkuu  wa Mkoa wa Geita, Meja  Janerali mstafu Ezekiel  Kyunga,  akifunga  mafunzo hayo aliwataka wachimbaji ,na  wamiliki  wa migodi  kuhakikisha wanakwenda kuboresha  utendaji kazi wao kwa weledi  kutokana  na mafunzo  waliopewa ili kudhibiti  ajali za mara kwa mara  migodini.

Alilitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuwasaidia  wachimbaji wadogo kuhakikisha wanawajengea  duka la kuuzia  dhahabu  na kuwaletea duka la vifaa vya  kisasa vya uchimbaji, zikiwamo kofia ngumu,  kifaa cha kuingiza hewa kurunzi.

Baadhi  ya washiriki  wa mafunzo hayo walimuomba Kyunga kupeleka kilio chao  kwa Rais John Magufuli  kuwa  kiwanda cha makenikia ya mchanga  ya dhahabu  kijengwe  katika kanda ya magharibi  kwa kuwa ndiyo inayozalisha dhahabu  kwa wingi.

Mwenyekiti  wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Geita ((Gerema), Christopher  Kadeo, aliwataka wachimbaji  kulipa  ada ya leseni kwa wakati  ili kuepuka kupokonywa  leseni.

Habari Kubwa