Wadai mil. 39/- fidia ujenzi kituo cha ukaguzi

14May 2017
Jumbe Ismaily
Nipashe Jumapili
Wadai mil. 39/- fidia ujenzi kituo cha ukaguzi

WANANCHI watano wa kijiji cha Muhalala, tarafa ya Chikuyu, wilayani Manyoni, mkoani Singida, wanadai zaidi ya Sh. milioni 39 za malimbikizo ya malipo ya fidia kupisha mradi wa kitaifa wa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa magari kinachojengwa katika kijiji hicho.

Wananchi hao walifafanua kuwa licha ya maeneo yao kuchukuliwa na serikali kwa ajili ya kupisha mradi huo, lakini kiasi cha malipo ya fidia waliyopokea ni kidogo ikilinganishwa na tathmini iliyofanywa na wataalamu wa mradi.

Walisema kuna baadhi ya malipo ya ardhi na miti ya matunda wamelipwa kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa, lakini pia kuna baadhi yao wamejikuta wakipokea kiasi pungufu cha malipo yaliyotathiminiwa huku wakiahidiwa suala lao kushughulikiwa kabla ya kuanza kwa mradi huo.

Mmoja wa walalamikaji hao, Aidani Njarika, alisema tathmini aliyofanyiwa kwenye ardhi ilikuwa na ukubwa wa ekari 55 .6 na kila ekari walikuwa wakilipwa Shilingi milioni moja, lakini fedha aliyopokea ni Sh. milioni 45 tu.

Benjamin Mlomba, alisema eneo lake lilikuwa na ukubwa wa ekari 19.27, lakini alilipwa saba na ekari 12 ambazo ni sawa na Sh. milioni 12 bado hajalipwa na alipofuatilia alielezwa kuwa kuna eneo ambalo halitatumika katika mradi huo na alipodai kurejeshewa eneo lake hakuwafanya hivyo.

Anderson Milimo, anayedai zaidi ya shilingi milioni moja, alisema kati ya maeneo manne aliyokuwa akidai, mawili alilipwa sawa na mengine mawili hakulipwa kama inavyostahili kwa mujibu wa tathimini aliyofanyiwa kwenye maeneo yake.

Dora Zakaria alisema eneo lake lenye ukubwa wa ekeri 3.5, alitakiwa kulipwa Sh. 300,000, miti mikubwa ya vivuli 35 na midogo 15, alilipwa 2,135,000 na anadai 1,500,000.

Mwananchi anayedai Sh. 13.900,000, George Kanyamala, alisema alikuwa na eneo la shamba lenye ukubwa wa ekari 9.90 na alilipwa Sh. 2,100,000, miti aina ya mipingo 35 ambayo alilipwa Sh. 4,500,000 na anadai Sh. 13,900,000 zikiwamo alizopunjwa kwenye ardhi.

Akizungumzia malalamiko ya wananchi hao, Ofisa Mtendaji wa kata ya Muhalala, Alex Mahanza,alikiri kupokea malalamiko ya wananchi hao na alichukua hatua ya kuandika barua kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Singida, lakini walipokwenda kukabidhi mradi kwa mkandarasi, walikabidhi eneo lote.

Kaimu Meneja wa Tanroads, Mkoa wa Singida, Injinia Johanes Mbegalo, alipotakiwa kuzungumzia malalamiko ya wananchi hao alikiri mkandarasi kukabidhiwa maeneo yote ya wananchi na kwamba hakuna mwananchi yeyote anayedai malipo ya fidia.

Akizungumza kwa njia ya simu Injini wa Kampuni ya NIMETA inayoshughulikia ujenzi wa kituo hicho, aliyejitambulisha kwa jina moja la Patrick, alisema wananchi wote wanaodai kupunjwa malipo yao watalipwa baada ya kufanyika kwa upimaji upya wa eneo hilo na itakapobainika kuna aliyepunjwa, serikali itawalipa.

Habari Kubwa