Wacharukia mbegu feki

02Jan 2018
Christina Haule
Nipashe
Wacharukia mbegu feki

TAASISI ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), imefungua kesi saba za changamoto katika mikoa mbalimbali nchini zinazowakabili wauzaji wa mbegu.

Kesi hizo zimeripotiwa kufuatia kuendelea kuuzwa mbegu feki na kusababisha wakulima kukosa kuona faida ya kilimo.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Patrick Ngwediagi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika kipindi cha mwaka 2016-2017 walifungua kesi hizo dhidi ya watu waliokuwa wanauza mbegu za mazao mbalimbali zisizo na ubora kwa wakulima.

 

Ngwediagi alizitaja mbegu hizo ni za nyanya, mahindi, pilipili hoho, vitunguu na mbogamboga kuuzwa kwa mkulima na kuzalisha mazao yasiyolingana na ukubwa wa eneo.

 

“Pia tuliweza kuwabaini wauzaji wa mbegu 70 waliokuwa wakiuza mbegu zisizokuwa na lebo ya kuonyesha ubora na zilizopitwa na wakati na zisizofanyiwa majaribio ya ubora maabara,” alisema.

 

Alisema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha wakulima hawauziwi mbegu feki msimu ujao wa kilimo kwa kutoa elimu kwa wakulima na umma kwa ujumla juu ya utambuzi wa mbegu halisi zenye ubora na zisizo na ubora au feki kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari, semina na mikutano.

 

Aidha, alisema kesi hizo zilifikishwa katika mahakama mbalimbali nchini ambapo washtakiwa wake wengine walilipa fidia kwa wakulima.

 

“Pia tumejipanga kutoa mafunzo ya uthibiti wa ubora wa mbegu kwa maofisa ugani kutoka wilaya zote za Tanzania,” alisema Gwediagi.

 

Naye mkulima wa Kibati wilayani Mvomero, Khamis Abdalah, alisema ni vyema TOSCI ikahakikisha wakulima wanapatiwa elimu zaidi ili kuwaepusha na kuchukua mbegu zisizofaa, hivyo kutoona faida ya kilimo.

 

Abdalah alisema ni vema wakaweka utaratibu wa kutoa elimu katika maduka ya pembejeo mara kwa mara ili waone umuhimu wa kuweka mbegu bora na kuwasaidia wakulima wasiuziwe mbegu zisizo na ubora ama kupata hasara.

Habari Kubwa