TPA yanunua vifaa kuongeza ufanisi Bandari ya Mtwara

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
TPA yanunua vifaa kuongeza ufanisi Bandari ya Mtwara

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imenunua vitendea kazi vipya na vya kisasa kwa ajili ya Bandari ya Mtwara, ili kuongeza ufanisi.

BANDARI MTWARA.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Ofisa Mawasiliano wa TPA, Leonard Magomba, vifaa hivyo ambavyo tayari baadhi vimeshawasili bandarini hapo ni pamoja na mzani wa kisasa (Movable Weigh Bridge)wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 ambao tayari unatumika.

Katika taarifa hiyo, ilielezwa kuwa vifaa vingine vilivyonunuliwa na vinavyotarajiwa kuwasili mwezi huu, ni pamoja na mashine za kubeba mizigo (Reach Stalker) mbili mpya zenye uwezo wa kubeba tani 40 kwa wakati mmoja. 

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, ndiye aliyetoa taarifa ya kununuliwa kwa vifaa hivyo wakati wa majumuisho ya ziara za Kamati za Bodi za Wakurugenzi wa TPA zinazoshughulikia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na Utekelezaji pamoja na Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara. 

Wakurugenzi wa bodi za kamati hizo ambazo ziliongozwa na Mwenyekiti Dk. Jabiri Bakari ni pamoja na Jayne Nyimbo, Renatus Mkinga, Aziz Kilonge na Jaffer Machano. 

"Kamati hizo zilitembelea miradi mbalimbali iliyopo Bandari za Mtwara na Lindi na kutoa maelekezo kadhaa ambayo ni muhimu katika kuendeleza bandari hizo, ili kuongeza huduma zake," Magomba alieleza katika taarifa yake hiyo. 

Taarifa hiyo ilimnukuu Mhandisi Kakoko akieleza kwa ununuzi wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa mipango ya kuifanya bandari hiyo kuwa ya kisasa zaidi. 

“Ununuzi wa vifaa tunaofanya sasa hivi utasaidia kuboresha na kuimarisha zaidi utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara na kuongeza ufanisi zaidi,” Mhandisi Kakoko alikaririwa katika taarifa hiyo. 

Ilielezwa zaidi katika taarifa hiyo kuwa vifaa vingine ambavyo mchakato wa manunuzi umeshafanyika ni pamoja na mzani mwingine wa pili wa kisasa (Movable Weigh Bridge) ambao pia una uwezo wa kupima hadi tani 100. 

Kwa mujibu wa Magomba, vifaa vingine vinavyotarajiwa kununuliwa kwa ajili ya bandari hiyo ni pamoja na boti maalum za kuhudumia mafuta (Mooring Boat) moja na boti moja ya ulinzi (Pilot Boat). 

Katika taarifa hiyo, Magomba pia alieleza kuwa mbali ya vifaa hivyo, Bandari ya Mtwara pia itapokea 'Terminal Tractors’ tisa ambayo ni matrekta maalum yanayovuta matrela yaliyopakiwa makontena au makontena yakiwa bandarini. 

Vilevile, Magomba alieleza katika taarifa yake hiyo kuwa Bandari ya Mtwara pia inatarajia kupokea mashine maalum ya kubebea makontena (Empty Container Handler), folklift mbili moja ya tani 16 na nyingine tani 20 pamoja na ‘Automatic Glab' moja ya tani 15. 

Magomba pia alieleza kuwa ikiwa ni sehemu ya ziara hiyo, Mhandisi Kakoko alifanya kikao na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mtwara na kuwaagiza kukutana na Mawakala wa Forodha wa Mtwara, ili kuwaelimisha umuhimu wa kutoa mizigo ya wateja kwa wakati. 

Magomba pia alieleza kuwa awali akitoa maelezo kwa Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi wa TPA inayoshughulikia Tehama na Utelekezaji, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA (Miundombinu) Mhandisi Karim Mattaka, alisema vifaa hivyo vitawasili Bandari ya Mtwara kuanzia mwezi huu. 

“Tunatarajia kuanza kuwasili kwa vifaa hivyo hapa Mtwara kuanzia Januari 2018, ili kuharakisha mpango kazi wetu wa kubadili bandari hii,” Mattaka alikaririwa. 

Katika taarifa yake, Magomba pia alisema Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Nelson Mlali, alisema kuna ongezeko la mizigo la wastani wa asilimia 16.5 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano. 

“Katika mwaka 2016/2017, Bandari ya Mtwara imehudumia wastani wa tani 377,590 za mizigo ambazo ni sawa na asilimia 93 ya uwezo wa bandari, ambapo uwezo wake ni kuhudumia ni tani 400,000 kwa mwaka," Mlali alikaririwa. 

Magomba alieleza katika taarifa yake kuwa kwa mujibu wa Mlali, ongezeko hilo limechangiwa zaidi na ongezeko la uzalishaji wa korosho ambalo ndilo zao kuu la biashara kwa mikoa ya kusini. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa mwaka 2017 pekee, Bandari ya Mtwara ambayo ina uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu hadi wa mita 211, imefanikiwa kusafirisha wastani wa tani 160,000 za korosho. 

Magomba alieleza katika taarifa hiyo kuwa Mlali alipongeza juhudi zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kuagiza korosho zote zisafirishwe kupitia Bandari ya Mtwara.

Taarifa ya Magomba pia ilimnukuu Mlali akieleza kuwa mbali ya korosho, Bandari ya Mtwara pia uhudumia shehena nyingine za mizigo kama vile saruji, mafuta na vifaa mbalimbali. 

 

Habari Kubwa