Tigo yatia neno viwango vya gharama 

31Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Tigo yatia neno viwango vya gharama 

KAMPUNI ya simu za mkononi ya  Tigo imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazodai wateja wake ndio wanaolipa fedha nyingi zaidi kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms).

Ofisa Mkuu wa Mawasiliano wa Tigo,  Jerome Albou.

Hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitoa ripoti ya robo ya tatu ya mwaka huu ikibainisha kuwa wateja wa mtandao huo hulipa zaidi kufanya mawasiliano kwa namna zote; iwe kupiga au kutuma sms ndani au nje ya mtandao au kufanya hivyo nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Mkuu wa Mawasiliano wa Tigo,  Jerome Albou,  alisema Tigo ni mtandao wa gharama nafuu zaidi nchini.

"Bando zetu zinaanzia Sh. 500; hakika wateja wa Tigo wanaonunua bando ya sauti ya Sh. 500 kupitia menu yetu mpya ya 147*00# wanapata dakika 16.

Pamoja na hili, wateja wa Tigo wanaonunua bando hii wanapokea bonasi ya dakika tano bure  kila mara wanaponunua bando hii kupitia promosheni ya tumekusoma ambayo inawapa jumla ya dakika 21," alisema Albou

Albou alisema Tigo inajulikana kwa promosheni kabambe na ubunifu wa ofa. Pamoja na kujijengea jina kama mtandao unaowaelewa zaidi wateja wake na kuwapa bidhaa zinazoendana na mahitaji ya soko.

Alisema wateja wa Tigo ndio watumiaji wa simu pekee wanaopokea bonasi za bure kwa kila bando wanayonunua, hivyo kuhakikisha wanafurahia huduma bora zaidi kwa viwango bora na nafuu nchini.

Alisema kupitia huduma zake za kipekee za sauti, ujumbe mfupi, intaneti yenye kasi na huduma za kifedha kupitia simu za mikononi, Tigo inaongoza kwa ubunifu wa kidigitali.

Aliongeza kuwa Tigo ndiyo kampuni ya simu kuzindua simu za Smartphone zenye lugha ya Kiswahili, pamoja kuzindua Facebook ya bure kwa lugha ya Kiswahili.

Alisema kwa miaka mitatu mfululizo, Tigo ndio kampuni ya simu inayokuwa kwa kasi zaidi nchini, na hivyo kuwa kampuni ya pili kwa ukubwa nchini na wateja zaidi ya 11 milioni. 

Habari Kubwa