Soko la kisasa kudhibiti utoroshwaji mifugo

01Jan 2018
Cynthia Mwilolezi
Nipashe
Soko la kisasa kudhibiti utoroshwaji mifugo

SERIKALI imeamua kudhibiti utoroshaji mifugo nje ya nchi kwa kujenga soko la kisasa katika Kijiji cha Oriendeke, wilayani Longido.

Ujenzi wa soko hilo utagharimu Sh. milioni 782 hadi kukamilika kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema kuwa lengo la ujenzi wa soko hilo ni kudhibiti uuzwaji holela wa mifugo unaofanywa na wajanja toka nchi jirani.

 

Alisema wilaya zilizopo mpakani na nchi ya Kenya kama Longido na Ngorongoro ni waathirika wakubwa wa kushawishiwa kuuza mifugo yao bila utaratibu hatua ambayo inaikosesha serikali mapato.

 

“Serikali haiwezi kupata mapato kama utaratibu huu ukiendelea, hivyo kupitia soko la uhakika wafugaji watapata eneo la kuuza kwa uhuru na kupata kipato kizuri, lakini serikali tutapata mapato yake,” alisema.

 

Kwa upande wa mapato ya utalii, alisema yameongezeka kutoka Sh. trilioni tatu, mwaka 2015, hadi zaidi ya Sh. trilioni nne, mwaka 2016, huku watalii nao wakiongezeka kutoka 1,200 mwaka 2015 hadi kufikia 1,400 hivi sasa.

 

Aidha, alisema serikali imeamua kupunguza changamoto ya mageti matatu na kuwa na geti moja, ili kupunguza kero kwa watalii.

 

“Lakini baada ya kuwa na geti moja Wilaya ya Longido, Monduli na Ngorongoro watakaa kupitia halmashauri zao watagawana mapato hayo kadri watakavyopata.

 

Aidha alisema huko mbele ni lengo la serikali kuondoa kabisa mageti hayo na kuangalia jinsi ya watalii watakavyolipa moja kwa moja halmashauri husika, ili kuondoa usumbufu wa vizuizi barabarani.

 

Habari Kubwa