Shein ajivunia matokeo ukusanyaji mapato

01Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Shein ajivunia matokeo ukusanyaji mapato

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato zimeiwezesha Serikali kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za 2015 ya kupandisha mishahara ya kima cha chini kwa asilimia 100 kutoka Shilingi 150,000 mpaka 300,000 kwa mwezi kwa watumishi wa Serikali.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Dk. Shein aliyasema hayo jana katika hotuba yake ya kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2018 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari Ikulu na kusisitiza kuwa serikali imeweza kuongeza pensheni kwa wastaafu na kuendelea kutoa fedha za pensheni ya jamii kwa wazee wote wanaostahiki.

 

Alieleza tangu Aprili, 2017 walengwa wa nyongeza hizo wamekuwa wakifaidika na neema hiyo ambapo pia, katika mwaka 2017 Serikali imezidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi wanaopata mshahara wa kima cha chini, jambo ambalo ni faraja kuona waajiri wengi katika sekta hiyo wameshaitikia wito licha ya kuwapo baadhi waliotaka kurejesha nyuma juhudi hizo za serikali.

 

Aliongeza uchumi wa Zanzibar unaendelea kuimarika na katika robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2017 (Januari-Machi), kasi ya ukuaji uchumi ilifikia asilimia 6.3 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 5.2 kwa kipindi kama hicho cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2016 ambapo katika kipindi cha robo mwaka ya pili (Aprili-Juni) kwa mwaka 2017 ukuaji wa uchumi nao uliimarika na kufikia asilimia 8.2.

 

Hivyo, Dk. Shein alieleza kuwa ni jukumu la kila mmoja katika mwaka 2018 la kuongeza juhudi ili kuhakikisha yanaendelea kutekelezwa vizuri malengo hayo yaliobainishwa kwenye MKUZA III na mipango mengine ya maendeleo.

 

Aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa juhudi zao za maendeleo ya kutia moyo yaliyopatikana katika sekta mbalimbali za maendeleo kwenye ziara za mikoa aliyofanya Unguja na Pemba zikiwamo sekta za kiuchumi na kijamii ikiwa ni katika kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA 111 na Malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.

 

Aidha, Serikali imepiga hatua kubwa  katika ujenzi wa miundombinu katika sekta ya afya na hivi sasa juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuimarisha huduma pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa vya utibabu katika hospitali na vituo vya afya.

 

Aliongeza katika mwaka wa fedha uliomalizika 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya Shilingi  bilioni 7.0 kwa ununuzi wa dawa na vifaa vya utibabu, sawa na ongezeko la asilimia 42.9 ikilinganishwa na kiwango kilichotengwa kwa mwaka 2016/2017.

 

Kwa upande wa sekta ya elimu, alisema serikali imeshaanza ujenzi wa mradi wa shule 9 za ghorofa katika sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba, ili kuimarisha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi hapa nchini ambapo ujenzi wa skuli hizo utagharimu jumla ya Sh. bilioni 24.4 ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa OPEC, dhamira ikiwa ni kumaliza ujenzi wa skuli hizo ifikapo Januari, 2019.

 

 

 

Habari Kubwa