Mvuvi afa maji, mwingine akatwa vidole

30Dec 2017
Jaliwason Jasson
Nipashe
Mvuvi afa maji, mwingine akatwa vidole

WAKATI mvuvi mmoja aliyedaiwa kuwa amelewa na kwenda kuvua samaki Ziwa Babati, akipoteza maisha kwa kufa maji, mkazi wa Kijiji cha Gallapo, amekatwa vidole vitatu vya mkono  wa kushoto wakati akiamua  ugomvi wa wanagombania  mwanamke  katika klabu ya pombe za kienyeji.

Ziwa Babati.

Kamanda wa Polisi  wa Mkoa wa Manyara,  Augustino Senga,  alithibitisha kutokea kwa matukio hayo mawili wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.

 

Alisema tukio la kukatwa vidole lilitokea Desemba 25, majira ya saa 5:45, asubuhi, katika klabu ya pombe za kienyeji kijijini hapo, wakati Hussen Abdalla (35), alipoamua kuingilia kati ugomvi wa wanaume waliokuwa wakigombea mwanamke.

 

Alisema watuhumiwa wote walifahamika kwa jina moja moja wakati mtuhumiwa wa kwanza alijulikana kwa jina la Mongoo na mwingine kwa Yohani.

 

Alisema walikuwa wakigombania mwanamke na Abdalla alipoingilia ugomvi huo, alikatwa vidole vitatu vya mkono wa kushoto.

 

Hata hivyo, alisema watuhumiwa bado hawajakamatwa, wanasakwa na polisi ili wafikishwe mahakamani.

 

Katika hatua nyingine, mvuvi mmoja alikutwa amekufa maji katika Ziwa Babati na mwili wake ukielea.

 

Kamanda Senga, alisema mvuvi huyo, Samweli Konki (35), alikwenda kuvua samaki wakati akiwa amelewa.

 

Alisema tukio hilo lilitokea Desemba 26, saa 8:00 mchana katika Kijiji cha Nakwa, wilayani Babati.

 

Kamanda Senga alifafanua kuwa  Konki alishauriwa  na ndugu zake asiende ziwani kuvua samaki  kwa kuwa alikuwa amelewa ili asije akazama, lakini alikaidi na kuwatoroka kwenda kuvua na mauti yalipomkuta wakati akivua samaki.

 

Wakati huo huo, polisi mkoani hapa, wamepiga marufuku uchomaji matairi na ulipuaji wa baruti na mafataki katika kusherekea    sherehe za kuupokea   mwaka mpya 2018, siku ya Jumapili.

 

Alisema  mtu yeyote atakayetaka kulipua fataki au baruti anatakiwa  kuomba kibali polisi.

 

Alisema wamejipanga vizuri  kusambaza askari  katika maeneo  mengi vijijini  ambao watakuwa  wamevaa sare zao na watakaokuwa wamevaa nguo za kiraia  ili kupambana na watu watakaotaka kuleta vurugu siku hiyo.

 

 

Habari Kubwa