Mvua yatibua usafiri treni mizigo Tanga

14May 2017
Steven William
Nipashe Jumapili
Mvua yatibua usafiri treni mizigo Tanga

MVUA mfululizo zinaoendelea kunyesha mfululizo na kusababisha mafuriko katika maeneo kadhaa ya mkoa wa Tanga zimezua janga jingine.

Baadhi ya mafundi wa TRL wakiwa kandoni mwa eneo la reli lilililoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika wilaya ya Muheza, Tanga, jana.
(Picha: Steven William)

Safari hii, mvua hizo zinazoelezewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuwa hazijawahi kurekodiwa tangu mwaka 1949, zimekata mawasiliano ya usafiri wa treni ya Shirika la Reli (TRL), ambao hutegemewa zaidi kwa usafirishaji wa mizigo mikubwa kutokea Tanga kwenda maeneo mengine nchini, hasa saruji kutoka kwenye kiwanda kilichopo mkoani humo.

Hali hiyo imejitokeza baada ya kubainika kuwa daraja mojawapo kubwa la reli hiyo, lililopo katika eneo la Muheza, limekatika kwa kuathiriwa na mvua na hivyo kutopitika kwa sasa.

Kabla ya tukio hilo lililotokea jana, tayari mvua hizo zilishasababisha mtikisiko wa kiuchumi na kijamii katika mkoa huo baada ya mafuriko kuzagaa katika baadhi ya maeneo, kuharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya barabara na madaraja, kuharibu mazao, kubomoa nyumba na pia kusababisha vifo vya jumla ya watu takribani kumi.

“Hili ni pigo kubwa kwa uchumi wa Tanga kwa sababu usafiri wa treni hurahisisha ubebaji wa mizigo mikubwa kama saruji itokayo mkoani hapa,” mmoja wa wananchi aliyekataa kujitambulisha jina aliiambia Nipashe katika eneo la ajali.

KILICHOTOKEA, TAHADHARI YA DC
Usafiri huo wa mizigo kwa njia ya reli kati ya Tanga na jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine umesitishwa baada ya kukatika kwa daraja hilo lililopo katika eneo la mto Amtico, wilayani Muheza.

Jana, mwandishi aliwashuhudia  mafundi wa TRL wakiendelea na kazi ya kukarabati kipande cha reli kilichoathirika katika eneo hilo la daraja.

Hata hivyo, hakukuwa na taarifa zaidi za kiufundi kuelezea undani wa kilichotokea na pia ni lini au wakati gani kazi hiyo ya ukarabati ingekamilika na kurejesha usafiri wa treni katika reli hiyo.

Akizungumzia tishio la mvua zinazoendelea kunyesha usiku na mchana wilayani kwake, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanasha Tumbo, alisema ni vyema wananchi walio katika maeneo ya bondeni waondoke haraka kujiepusha na madhara zaidi badala ya kusubiri maafa zaidi yawakute.

Alisema wapo baadhi ya watu walioanzisha makazi kwenye maeneo hatarishi yasiyoruhusiwa kisheria yakiwamo hayo ya bondeni na hivyo, wanatakiwa kuondoka mara moja kabla hatua za kuwaondoa kinguvu pia kutumika.

Maeneo ambayo nyumba za makazi zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kujaa maji kiasi cha wananchi waliokuwa wakiishi kukosa mahala pa kuishi kwa sasa ni pamoja na wale waliojenga kandoni mwa mto Amtco ambao umefurika kiasi cha kutapisha maji yake nje.

Hivi karibuni, TMA iliwatahadharisha wananchi nchini kote kuwa wawe waanagalifu ikiwa ni pamoja na kujiondoa katika nyumba za bondeni kwa sababu mvua inayoendelea kunyesha mfululizo katika maeneo mbalimbali nchini inatarajiwa kudumu hadi mwishoni mwa Mei.

Habari Kubwa